Wananchi waige Busega ujenzi hosteli za wasichana

GAZETI hili hivi karibuni lilichapisha habari ya kusikitisha yenye kichwa cha habari: “Wanafunzi wengi wa kike Busega wakatisha masomo yao kwa mimba.’’ Habari hiyo pia ilitoa takwimu kwamba kila wanafunzi 40 wanaojiunga na kidato cha kwanza wilayani Busega mkoani Simiyu kila mwaka, kati yao 15 hadi 18 hukatishwa masomo yao kwa sababu ya kupata ujauzito.

Hakuna ubishi kwamba kama hali hiyo haitatafutiwa suluhisho la kudumu, watoto wengi wa kike katika wilaya hiyo wataendelea kukatishwa tamaa katika harakati za kutimiza ndoto zao za kuwafikisha katika elimu ya juu na kupata ujuzi wa kuwasaidia maishani mwao, kama ilivyo wenzao wa kume.

Hapa tunapenda kumpongeza Mbunge wa Jimbo la Busega, Dk Raphael Chegeni kwa kushirikiana na viongozi wenzake jimboni humo, kuliwekea mkakati wa kukabiliana vilivyo tatizo hilo kwa watoto wetu wa kike.

Bila shaka sababu ziko nyingi, lakini sababu ya kukosa mabweni au hosteli na kusababisha wanafunzi wa kike kutembea umbali mrefu kwenda na kurudi shuleni, ina mchango mkubwa katika kufanikisha nia ovu ya wanaume wanaopenda kuwarubuni wanafunzi kwa kutumia shida na udhaifu walionao ili kuwaharibia maisha yao ya kitaaluma.

Mkakati wa Dk Chegeni wa kujenga hosteli za wasichana kwa shule ya sekondari zilizopo pembezoni mwa jimbo hilo, ziungwe mkono kwa kila hali ili kunusuru watoto wa kike wilayani humo kukosa elimu, ambayo ni ufunguo wa maisha.

Tunafarijika kupata taarifa kwamba tayari mradi huo wa ujenzi wa hosteli za wasichana, umeshaanza kutekelezwa katika shule ya sekondari ya Ngasamo; na kwamba zingine nne za Mkula, Malili, Kabita na Sogesca ziko mbioni kutekeleza mradi huo.

Tunawapongeza wananchi wa jimbo la Busega, wadau na washirika wa maendeleo kwa kuunga mkono juhudi za utekelezaji mradi huo ili ufikie lengo lake la kuwapatia malazi karibu na shule zao wanafunzi wa kike.

Tatizo la ukosefu wa hosteli au mabweni ya wasichana, halipo katika jimbo la Busega peke yake, bali pia majimbo na mikoa mingine hapa nchini. Hali kama hiyo ya wasichana kuingia katika vishawishi vya ngono na hatimaye kuishia kupata ujauzito, lipo pia katika maeneo hayo mengine.

Wakazi wa jimbo la Busega wameonesha mfano wa kukabiliana na tatizo hilo. Hivyo tungependa pia wananchi wa maeneo mengine nchini, yenye tatizo kama hilo la wanafunzi kupata mimba kutokana na sababu za kuishi mbali na maeneo ziliko shule wanazosoma, waweke katika mipango yao ya maendeleo ya jamii, miradi ya ujenzi wa hosteli za wasichana.