Shule hii ipatiwe walimu, miundombinu haraka

GAZETI hili jana lilichapisha habari iliyobeba kichwa cha habari ‘Walimu wanne wafundisha wanafunzi 380.’ Ni shule ya Msingi Makongolo iliyopo Kata ya Magamba Manispaa ya Mpanda mkoani Rukwa.

Shule hiyo yenye wanafunzi wa awali na wa shule ya msingi hadi darasa la nne ina vyumba viwili tu vya madarasa, matundu mawili ya vyoo vya wanafunzi huku walimu wao wakiwa hawana choo, hivyo kulazimika kutumia choo cha nyumbani kwa Mwalimu Mkuu.

Ni kama hadithi vile, lakini ni ukweli pia kwamba shule hiyo iliyopo umbali wa kilometa 10 kutoka Mpanda Mjini kwa barabara ya lami, walimu wake hawana ofisi na hivyo kufanya kazi zao chini ya miti shuleni hapo huku wanafunzi wakifundishwa kwa zamu.

Tunapenda kwanza kutoa pongezi kwa walimu hao wanne, kuendelea kuchapa kazi licha ya mazingira magumu ya kazi waliyonayo wao pamoja na wanafunzi wao. Ni kama vile kampeni ya kitaifa ya kuboresha mazingira na miundombinu ya shule za msingi, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa madarasa na utengenezaji wa madawati, haikupita katika Manispaa ya Mpanda hususani katika shule hiyo.

Tunapenda kutoa mwito maalumu, kwanza kwa wahusika wa moja kwa moja wa Idara ya Elimu kutoka ngazi za Kata na Manispaa, kuchukua hatua za makusudi kwa kushirikiana na uongozi wa manispaa ya Mpanda, kupata taarifa zaidi juu ya hali ya shule hiyo, ufinyu wa miundombi pamoja na uhaba mkubwa walimu ambao unatia shaka utoaji wa elimu bora kwa wanafunzi hao.

Katika habari husika ilidokezwa pia kumepatikana wafadhili wa Kampuni ya Ujenzi ya China, inayokarabati barabara ambayo iliahidi kuipatia shule hiyo matofali 400 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, lakini inadaiwa ni matofali 40 tu ndiyo yaliyofikishwa shuleni hapo.

Haihitajiki nguvu ya ziada kubaini kwamba kuna kitu si sawa katika suala hili kwa maana ya matofali, kushindwa kufika shuleni hapo kwa ajili ya kukamilisha dhamira ya awali ya kujenga vyumba vya madarasa.

Kwa tukio hili, uongozi wa idara ya elimu pamoja na uongozi wa shule na serikali, uhakikishe unalifanyia uchunguzi suala hilo pia ili wafadhili waliojitolea kwa jambo hili muhimu kwa miundombinu ya shule, wasikatishwe tamaa kwa mbinu chafu za watu wachache kujinufaisha kutokana mchango huo.

Hapa tunapenda pia kutoa mwito kwa wazazi wa watoto, wanaosoma katika shule kama hiyo, wajitahidi kujielimisha juu ya mazingira wanayosoma watoto wao ili nao waweze kutoa mchango wao na kushiriki kikamilifu katika kuchangia maendeleo endelevu ya shule, kwani tunaamini kwamba kama wazazi wangejihusisha pia, hali hiyo huenda isingefika katika hali hii ya sasa.