Wenye magazeti nchini nendeni haraka Maelezo

AGOSTI 23 wiki hii serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO) iliuarifu umma kuhusu kuanza upya utoaji wa leseni kwa magazeti na majarida nchini. Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi, hatua hiyo ni utekelezaji wa matakwa ya Kifungu cha 5(e) cha Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016.

Kwamba kwa mujibu wa sheria hiyo, serikali inatakiwa kuanza kutoa leseni za machapisho mbalimbali, ikiwemo magazeti na majarida yote nchini. Tunapongeza hatua hiyo kwa sababu utoaji wa leseni hizo, unafanyika kwa mujibu wa Kanuni ya 7 ya Sheria ya Huduma za Habari za mwaka 2017, zilizochapishwa kwa mujibu wa tangazo la Serikali Namba 18 la Februari 3 mwaka huu.

Utaratibu huu wa sasa unafuta mfumo wa awali wa utoaji wa Hati za Usajili wa Magazeti na Majarida, uliokuwa ukitumika kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 ambayo imefutwa.

Kwa mujibu wa Dk Abbasi, utaratibu huu mpya utawahusu wamiliki wote wa magazeti (newspapers), majarida (journals, magazines na newsletters) na wamiliki wapya ambao hawakuwa wameyasajili machapisho yao.

Aidha leseni hizi zitahuishwa kila mwaka, kwa mujibu wa Kanuni za 8(3) na 12(1)(2) za Kanuni za Sheria ya Huduma za Habari, 2017. Tunahimiza wamiliki wa magazeti kwenda haraka MAELEZO kuchukua fomu za maombi, ambapo Dk Abbasi anafafanua kuwa fomu za maombi pamoja akaunti ya kulipia na orodha ya nyaraka zinazohitajika kwa ajili ya usajili, vinapatikana katika ofisi za MAELEZO Dar es Salaam na Dodoma; au katika sehemu ya “Huduma Zetu” katika tovuti ya www.maelezo.go.tz.

Dk Abbasi anaeleza kuwa wamiliki wa magazeti na majarida ambao wana usajili wa zamani, wanatakiwa kuanzia Agosti 23 hadi Oktoba 15, 2017 wawe wamekamilisha taratibu na kupatiwa leseni mpya za uendeshaji na uchapishaji wa majarida na magazeti.

Kwamba baada ya muda huo hawataruhusiwa kuyachapisha, kwani watakuwa wametenda kosa kisheria. Tunawasihi wamiliki wa magazeti ya zamani na majarida, waache kusubiri siku za mwisho, ndipo watekeleze suala hilo.

Kwa wale wanaotaka kusajili magazeti mapya na majarida, nao tunawahimiza waende haraka MAELEZO hivi sasa kufanya usajili huo, ambao ulikuwa umesitishwa. Aidha, tunawasihi wahusika wote kuwa makini mno na usajili huu wa sasa, unaofanyika chini ya sheria mpya.