Wakulima wekeni akiba ya mahindi

MWAKA huu umekuwa na neema kwa kuwa maeneo mengi nchini yalipata mvua na hivyo kuwa na wingi wa mazao.

Tunasema ulikuwa na neema kwa kuwa mazao mengi ya chakula yalistawi vyema likiwemo zao la mahindi ambalo hutumiwa na makabila karibu yote hapa nchini, lakini tunatoa ushauri kwa wakulima kuweka akiba kwa ajili ya nyakati zijazo.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili juzi mkoani Rukwa katika soko la wakulima la Mandela lililopo Kata ya Mazwi, Manispaa ya Sumbawanga ulibaini kuwa, mahindi yamefurika sokoni huku bei ya rejareja ikiwa imeshuka kwa kasi. Kumbe hata wale ambao hawakulima, ni muda mzuri wa kununua na kuweka akiba nyumbani.

Katika uchunguzi huo bei ya jumla na rejareja ya mahindi mkoani humo imeporomoka kutoka Sh 110,000 kwa gunia lenye ujazo wa kilo 100 lililokuwa likiuzwa miezi mitatu iliyopita hadi kati ya Sh 43,000 na 30,000 Wakati bei ya zao hilo ikiwa imeporomoka katika mkoa wa Rukwa, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe amewataka madiwani kushirikiana na serikali kuhamasisha wananchi ili wasiuze chakula cha ziada hasa mahindi waliyovuna kwa wingi katika msimu huu.

Gondwe alisema hayo katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kilichofanyika mwishoni mwa wiki. Alisema katika siku za hivi karibuni ameshuhudia idadi kubwa ya malori pamoja na wafanyabishara kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini wanaofika vijijini kwa wananchi kununua mahindi na kuyasafirisha nje ya Handeni.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Ramadhani Diliwa alisema ipo haja kwa viongozi wote kuendelea kuwahamasisha wananchi kwenye maeneo yao kuhusu umuhimu wa kuhifadhi chakula ili kudhibiti njaa kwenye kaya.

Tunataka kutumia ushauri wa DC Gondwe na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo kwa viongozi wengine kote nchini na Watanzania wote, kuweka akiba ya mahindi na mazao mengine katika kipindi hiki, kwa ajili ya siku zijazo.

Kama nchi, bado tunategemea kilimo cha msimu wa mvua badala ya umwagiliaji, ni vema kuweka akiba kwani hatuna uhakika kama mvua hiyo iliyotuwezesha kuvuna mwaka huu, itakuwa vile vile na mwakani.