Mkakati huu uigwe miji yote Afrika Mashariki

MKAKATI wa Mamlaka ya Jiji la Kigali wa kutaka kuzuia magari ya watu binafsi, kuingia katikati ya jiji ili kukabiliana na foleni na msongamano, hauna budi kupongezwa. Tunashauri mamlaka za miji mingine katika Afrika Mashariki, kuchukua hatua hiyo muhimu.

Nia kubwa ya mkakati huo ni kuondoa msongamano, lakini kubwa zaidi ni kurahisisha shughuli za maendeleo kufanyika kirahisi. Miji mingi ya Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla, inakabiliwa na msongamano mkubwa wa magari.

Katika nchi zilizoendelea, miji mingi hairuhusu magari binafsi kuingia katikati na badala yake, usafiri wa umma hasa wa treni ndiyo unaotumika. Hatua inayotaka kuchukuliwa na Mamlaka ya Kigali ni suluhisho kubwa la foleni ambayo imekuwa ni kikwazo kikuu cha uchumi, kwani wafanyakazi na wafanyabiashara hutumia muda mwingi barabarani, badala ya kuwa kwenye maeneo yao ya kazi.

Kwa kuonesha dhamira dhahiri ya mkakati huyo, tayari baadhi ya barabara za Jiji la Kigali, zimeanza kupanuliwa, lengo likiwa kuruhusu magari ya umma kufanya kazi kwa ufanisi ifikapo katikati ya mwaka ujao.

Katika kusisitiza hilo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Jiji hilo la Kigali, Bruno Rangira, amesisitiza kuwa timu ya wataalamu wako kazini, kuhakikisha suala la usafiri wa umma unapewa kipaumbele katika jiji hilo.

Katika mipango ya jiji hilo, njia tano maalumu kwa ajili ya mabasi tu, zinazotarajiwa kuwa na urefu wa kilometa 92, zitaanza kujengwa hadi kufikia mwaka 2026. Dar es Salaam tayari kuna Mradi wa Magari Yaendayo kwa Haraka (DART), ambao ni sehemu ya mkakati kama huo ambao umepunguza kwa kiasi fulani msongamano na bado haujakamilika.

Tunaamini ukikamilika, Jiji la Dar es Salaam litakuwa limepunguza kwa kiasi kikubwa msururu mkubwa, ambao umekuwa ukiathiri uchumi wa wakazi wa mji huo. Pia katika jiji la Dar es Salaam kuna treni za ruti ndogo, kutoka Stesheni, iliyopo katikati ya jiji, kwenda Ubungo na Pugu nje kidogo ya jiji, ambazo zimesaidia kupunguza msongamano wa magari.

Lakini, mamlaka za jiji la Dar es Salaam, bado hazijafikia hatua ya kuzuia magari binafsi kuingia katikati ya jiji, kwa kuwa kuwepo kwa magari yaendayo kwa haraka na treni hizo ndogo, hakujakidhi mahitaji ya wakazi wa mji huo, wapatao 4,364,541, kwa hesabu ya Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika mwaka wa 2012. Tunashauri mamlaka za miji za Afrika Mashariki, kuiga mfano wa Kigali ili kuziwezesha kupunguza au kuondoa tatizo la msongamano unaozikabili.