Polisi Dar kazeni uzi kudhibiti daladala

SERIKALI ya Awamu ya Tano inajitahidi mno kuboresha barabara katika mikoa mbalimbali nchini. Mathalani, katika jiji la Dar es Salaam kuna barabara nyingi za mitaani, zinaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami hivi sasa na nyingine kadhaa zimeshakamilika.

Hata hivyo, sekta ya usafirishaji wa abiria jijini Dar es Salaam inatiwa doa na trafiki na makondakta na madereva wa daladala. Kwa upande wa trafiki, wao wanalaumiwa kwa kusababisha foleni kwenye taa za Tazara, Keko na Ubungo.

Wananchi wanadai kuwa trafiki wanaruhusu magari kwa upendeleo, hivyo mara nyingi kusababisha foleni. Jambo lingine kuhusu trafiki ni kushindwa kuingia ndani ya daladala na kukagua uozo uliopo.

Daladala nyingi zimechakaa na kuoza ndani, kuanzia viti, paa na bodi. Lakini, mara nyingi trafiki wamekuwa wakikagua nje ya daladala na ‘kumalizana’ na madereva na makondakta haraka haraka.

Humo ndani ya daladala, kuna tatizo sugu la makondakta wengi kutotoa tiketi. Hata wale wachache wanaotoa tiketi, tiketi nyingi ni feki. Trafiki hawakagui tiketi hizo wala hawaingii ndani ya daladala, kukagua abiria kama wote wana tiketi.

Makondakta wengi wa daladala ni walanguzi wa tiketi, wanaoibia wamiliki wa magari na serikali kwa ujumla. Kwa mfano, daladala zinazotoka Mbezi kwenda Mlandizi, Kibaha na Chalinze, zinatoza abiria wanaokwenda Kibaha Mailimoja Sh 800.

Lakini, nauli halali ya kutoka Mbezi hadi Kibaha Mailimoja, iliyotangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchikavu na Majini (Sumatra) ni Sh 500 tu. Hivyo, kwa ulanguzi wanaofanya makondakta, kila abiria anaibiwa Sh 300 akikata tiketi kila siku.

Huu ni wizi mkubwa! Tuna imani trafiki watafuatilia daladala za ruti hiyo na kukamata makondakta na madereva wote wanaovunja sheria. Suala lingine ni uchafu wa makondakta.

Tunampongeza Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Awadhi Haji aliyeanzisha hivi karibuni operesheni ya kukamata madereva na makondakta wachafu.

Kwa mujibu wa Haji, operesheni hiyo imelenga kuwafanya makondakta na madereva wa daladala, kuwa nadhifu hivyo kuondoa kero ya uchafu na harufu mbaya, wanayoisababisha kwa abiria.

Awadhi anasema dereva au kondakta akikamatwa ana sare chafu, anapigwa faini na pia mmiliki wa gari, anaitwa ili alete sare mpya pamoja na risiti zake. Pia kwamba kama sare ni safi lakini ‘amejijaradia juu kwa juu’, anavuliwa hizo na anavalishwa sare mpya.

Tunasihi Jeshi la Polisi kukaza uzi kuendelea na operesheni hiyo mpaka madereva na makondakta wote wa daladala, watakapobadilika na kufanya shughuli za usafirishaji wa abiria kwa kuzingatia kanuni na sheria.