Hongera taasisi ya Moyo ya JKCI kwa kazi nzuri

MOJA ya habari zilizochapishwa katika gazeti hili leo ni pamoja na ile ya kazi nzuri ya matibabu ya ugonjwa wa moyo inayofanywa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa Watanzania, raia wa Afrika Mashariki na bara la Afrika kwa ujumla.

Taasisi hiyo iliyoanzishwa mwaka 2015, hivi sasa inaendelea kujizolea sifa za kutoa tiba sahihi kwa wagonjwa wa moyo, tofauti na hapo awali ambapo wagonjwa wanaokabiliwa na tatizo hilo walikuwa wanasafirishwa kwenda kutibiwa nje ya nchi hususani nchini India kwa gharama kubwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi anasema tangu kuanzishwa kwake tayari jumla ya wagonjwa wapatao 1,500 wameshatibiwa na taasisi hiyo tena kwa gharama nafuu kiasi cha kukoa Sh bilioni 45.

Nchi nyingine zinazonufaika kupata matibabu katika taasisi hiyo ni pamoja na Kenya, Comoro, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na kwamba sasa kwa mujibu wa Profesa Janabi, taasisi yake inategemea kuwapokea wagonjwa pia kutoka nchi za Malawi na Zambia.

Tunapenda kuungana na Watanzania wenzetu kuipongeza taasisi ya JKCI kwa utendaji kazi kwa weledi unaostahiki kiasi cha kujiletea sifa siyo kwa Watanzania tu peke yake bali hata toka nchi nyingine zinazopata matibabu hayo hapa nchini hivi sasa na kwa siku za usoni.

Hapa tungependa kutoa mwito maalumu kwa wafanyakazi wa taasisi hiyo kuongeza bidii katika kazi zao bila kusahau uzalendo kwa nchi yao kwa kuwa mabalozi waziri wakati wa utekelezaji majukumu yao ya kazi.

Huduma ya matibabu hayo nyeti tuliyokuwa tunaipata nje ya nchi, hivi sasa tunaendelea kuipata hapa nchini huku wafanyakazi wazawa wa taasisi hiyo wakiwa ni asilimia 70 na asilimia 30 tu ndiyo wanaotoka nje ya nchi yetu.

Hayo ni mafanikio makubwa katika sekta hiyo ya afya na hatuna budi kujivunia kwa kila hali. Lakini pia tunapenda kuungana na Mkurugenzi Profesa Janabi kwa kuwasihi wanawake wajawazito nchini kwenda katika taasisi hiyo kupimwa usalama na afya kwa watoto wanaotarajia kujifungua kuwanusuru na matatizo ya moyo.

Umuhimu wa kuchukua hatua hiyo kwa mujibu wa Profesa Janabi unatokana na ukweli wa takwimu ambao unaonesha kuwa kati ya watoto milioni moja wanaozaliwa Tanzania kwa mwaka, 100,000 kati yao hukutwa na matatizo ya moyo. Anasema hatua hiyo itasaidia kujua mapema endapo mtoto ana tundu la moyo na hivyo kabla hajazaliwa wataalamu watakuwa tayari wameshaandaa matibabu yake.