Utamaduni wa kukabidhiana uongozi urithiwe nchi za EAC

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) ni miongoni mwa jumuiya makini na chache, zinazoaminika barani Afrika na duniani kwa ujumla.

Ni jumuiya inayolenga kuwakomboa watu wake zaidi ya milioni 150 kutoka katika lindi la umasikini na kuwafi kisha kwenye maendeleo endelevu. EAC ina nchi wanachama sita ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini.

Nchi zote hizo ni huru na zinajitahidi kutumia misingi ya kidemokrasia kwa maana ya kufanya uchaguzi ili kuweza kupata viongozi wa wao kwa amani na utulivu. Lakini ni ukweli pia kwamba bado kuna ukakasi ndani ya nchi za EAC na nchi nyingine za Afrika, juu ya namna ya kuachiana uongozi wa ngazi ya juu kwa maana ya marais, wanapohitimisha muda wao wa kikatibu.

Tunapenda kwanza kuchukua fursa hii kuzipongeza nchi za Tanzania na Liberia, kwa kujenga na kuuendeleza kwa makusudi utamaduni wa kidemokrasia wa kuachia madaraka ya juu ya nchi kupitia uchaguzi na hatimaye anayechaguliwa na wananchi, ndiye anayekabidhiwa kijiti cha uongozi.

Hapa ni vizuri kukumbushana kwamba Baba wa Taifa la Tanzania, hayati Mwalimu Julius Nyerere alipong’atuka nafasi ya urais mwaka 1985 baada ya kuiongoza nchi kwa miaka 23, kupitia demokrasia ya uchaguzi alimwachia madaraka Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi.

Naye kupitia utamaduni huohuo, alimwachia Rais Benjamin Mkapa kuongoza Awamu ya Tatu na kufuatiwa na Rais Jakaya Kikwete wa Awamu ya Nne na kisha kukabidhi kwa Rais wa sasa, Dk John Magufuli wa Awamu ya Tano.

Pamoja na tofauti zao za kisiasa, kikabila, kiitikadi na kidini, Watanzania wanaheshimu utamaduni huu kwa umakini unaostahiki. Utamaduni huu mzuri, pia umechukuliwa na anayemaliza muda wake wa uongozi nchi Liberia, Rais Ellen Johnson Sirleaf aliyeongoza nchi hiyo kwa miaka 12 mfululizo kwa kuchaguliwa kwa awamu mbili za miaka sita sita kila moja.

Mama huyo ambaye anaingia katika historia ya Afrika kuwa rais wa kwanza mwanamke kuchaguliwa kwa kura, yuko tayari kuendeleza utamaduni huu mzuri kwa kusubiri sasa kumkabidhi atakayechaguliwa na wananchi wa nchi yake ili amkabidhi kijiti cha uongozi.

Sisi tunapenda kutoa mwito kwa nchi zote wanachama wa EAC, kuupokea na kuuendeleza utamaduni huu wa kupokezana vijiti vya uongozi, kwa mujibu wa katiba za nchi husika ili kutoa nafasi kwa wananchi wa kanda hiyo, kukabiliana na umasikini badala ya migogoro ya kusaka madaraka.

Tunaamini kwamba mifano hai hiyo miwili, inaweza kuwa kioo kwa viongozi wetu ili kuendeleza kwa makusudi utamaduni wa amani na utulivu wa kubadilishana uongozi wa nchi.