Trafiki waondolewe mataa ya kuongozea magari Dar

JUZI Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo alitembelea vituo vya Morocco na Kivukoni vya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam.

Baada ya ziara yake hiyo, Jafo alizungumza na waandishi wa habari, ambapo alieleza kwa undani kero zilizopo na kutoa maagizo kadhaa na mojawapo linahusu askari wa kikosi cha usalama barabarani (trafiki).

Kwanza, tunamuunga mkono Waziri Jafo kwa kumwagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka, Ronald Lwakatare kuwasiliana na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani cha Jeshi la Polisi, kuangalia uwezekano wa kuruhusu taa za kuongozea magari zilizo kwenye mfumo, zifanye kazi hiyo badala ya kazi hiyo kufanywa na trafiki.

Kwa mujibu wa Jafo, kitendo cha askari kuongoza magari katika barabara za mfumo huo, kinasababisha magari hayo kutofika vituoni kwa wakati. Jafo anasisitiza kuwa ni vema taa za kuongozea magari barabarani, zitumike ili mfumo wa Mabasi Yaendayo Haraka uweze kukidhi malengo yaliyokusudiwa.

Ni wazi kuwa Jafo alifikia hatua ya kutoa agizo hilo kutokana na serikali kupata malalamiko mengi ya wananchi kuhusu mabasi hayo kutofika vituoni kwa wakati. Wananchi wamekuwa wakidai kuwa kuchelewa kwa mabasi hayo vituoni, kunatokana na mfumo wa magari hayo kuingiliwa na trafiki, wanaoongoza magari katika taa.

Ikumbukwe kuwa wananchi wanategemea mno mradi huo, ambao umekuwa mkombozi kwao, hivyo haitakiwi wakae vituoni muda mrefu kusubiri mabasi. Kuwafanya wananchi wasubiri vituoni muda mrefu, kuna athari mbalimbali kiuchumi na kijamii. Kiuchumi, wanachelewa kwenda kuzalisha mali na kuongeza kipato katika maeneo yao.

Hali kadhalika, kuwachelewesha watu vituoni na kuwafanya walundikane, kiusalama siyo jambo zuri. Jambo lingine la kukumbuka ni kuwa wakati mradi wa mabasi hayo unaanza, wananchi walielezwa kuwa mabasi yatakuwa yakikaa vituoni muda mfupi mno kushusha na kupakia abiria.

Hivyo, kitendo cha mabasi hayo kuchelewa kufika vituoni katika muda uliopangwa hivi sasa ni kwenda kinyume cha malengo ya mradi. Awamu ya kwanza ya mradi huo ilianza kufanya kazi Mei 10, 2016 na hadi sasa mradi unasafirisha abiria zaidi ya 200,000 kwa siku.

Tuna imani kuwa agizo hilo la Jafo, litatekelezwa haraka kwa kuwaondoa trafiki katika taa za kuongezea magari kwenye maeneo ya mradi huo. Lakini, pia tunashauri trafiki wote katika mataa mengine ya kuongozea magari jijini Dar es Salaam, nao waondolewe, badala yake zitumike tu taa za kuongozea magari, kwani zipo za kutosha na nyingi zinafanya kazi.

Halmashauri za Dar es Salaam zishirikiane na Wakala wa Barabara (Tanroads), kutengeneza taa zote za kuongozea magari ambazo ni mbovu. Tunasisitiza kuwa trafiki wabakie barabarani, kufanya majukumu yao kipolisi tu; na siyo kufanya kazi ya kuongoza magari, kwani uzoefu unaonesha wamekuwa wakisababisha foleni zisizoisha, wakati mwingine wamekuwa wakifanya kazi kwa upendeleo na wengine wanachukua hongo.

Kwa ujumla, tunaiomba serikali ifuatilie kwa karibu na kila siku utendaji kazi wa mradi wa mabasi yaendayo haraka na kutatua kero zake. Huu ni mradi nyeti unaohitaji usimamizi wa hali ya juu!.