Tunamtakia kila la heri Rais Kenyatta

RAIS John Magufuli ni kati ya wakuu 20 wa nchi, ambao leo wanashuhudia sherehe ya kuapishwa kwa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Naibu Rais, William Ruto. Kwa mujibu wa Mkuu wa Utumishi wa Umma nchini humo, Joseph Kinyua, Kenyatta ataapishwa kwenye Kituo cha Kimataifa cha Michezo Moi, Kasarani, kuanzia saa nne asubuhi.

Kiapo hicho kitaongozwa na Msajili Mkuu wa Mahakama, Anne Amadi na kushuhudiwa na Jaji Mkuu wa Kenya, David Maraga. Sherehe hizo zinatarajiwa kugharimu Sh milioni 300 za Kenya.

Tuna kila sababu ya kumtakia kila la heri Rais Kenyatta na Naibu Rais, Ruto, kwa kuwa wameonesha ukomavu wa kisiasa, ushapavu, uvumilivu na ustahimilivu wa hali ya juu hasa kutokana na kutangazwa washindi mara mbili, kufuatia kesi zilizokuwa zinafunguliwa na vyama vya upinzani.

Pia tunawasihi viongozi hao wa upinzani, kukubali matokeo ili kujenga nchi kwa pamoja, badala ya kuendeleza mabishano, ambayo yanaweza kuzorotesha juhudi za serikali ya Kenya kuwahudumia wananchi wake.

Tunasema Kenyatta ameonesha ukomavu wa kisiasa, hasa kutokana na ahadi yake kwamba yeye ni Rais wa Wakenya wote, hata ambao hawakumpigia kura Oktoba 26. Amesema hatambagua au kumwadhibu yeyote, kwa sababu za msimamo wake wa kisiasa.

Moja ya vipaumbele vyake, cha kwanza ni amani kwa Wakenya wote na pili kuhakikisha umoja wa Wakenya wote, unakuwa msingi wa kupata maendeleo wanayoyataka. Kwake yeye, kushindania madaraka ni moja ya mhimili muhimu wa demokrasia, ilimradi ushindani huo usiwe kwenye misingi ya ukabila au eneo analotoka mtu, bali ulenge katika kuboresha maisha ya Wakenya.

Anaamini kwamba katika ushindani wowote, kuna washindi na walioshindwa, lakini kwamba kwenye uchaguzi wa Kenya, wote ni washindi. Akaongeza kwamba baada ya ushindani wa kisiasa, ni wajibu wao wote kuungana ili kuijenga nchi yao kwa pamoja.

Anasema kwenye siasa ni kawaida kuwa na tofauti za kisiasa, lakini hilo halimaanishi kwamba hawawezi kuwa pamoja na kuishi pamoja kwa amani. Kwa mujibu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), uchaguzi unaomweka Kenyatta madarakni leo, ulikuwa huru na wa haki, unaoaminika na wenye mafanikio kwenye mazingira magumu huku ikisisitiza kwamba Kenyatta atazingatia suala la amani, mafanikio, matakwa ya Katiba na mapatano.