EAC iendelee kusaka suluhisho la amani nchini Burundi

AWAMU ya nne ya mazungumzo ya mgororo wa Burundi, yalifanyika kati ya Novemba 27 na Desemba 8, mwaka huu mjini Arusha, Tanzania chini ya Msuluhishi wa mgogooro huo, Rais wa zamani wa Tanzania, Benjamin Mkapa yamemazilika bila kufi kiwa muafaka.

Taarifa kutoka ofisi ya msimamizi wa mazungumzo hayo, imeeleza wazi kwamba pande zinazopingana nchini Burundi, zimekataa kubadili misimamo yao na hivyo mazungumzo kusimamishwa bila kufikiwa muafaka wowote.

Hata hivyo, pamoja na hali hiyo, Msimamizi wa Mazungumzo ya Mgogoro huo, Mzee Mkapa amezisihi pande zote zinazoshiriki mazungumzo hayo kuacha vurugu na kauli za chuki na badala yake wafikirie jinsi ya kujenga umoja na mshikamano kwa faida ya Burundi na Warundi wote.

Hakuna ubishi kwamba kukwama kwa mazungumzo hayo, kunatoa taswira isiyoridhisha kwa viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambao walitarajia kwamba ndugu zetu wanaovutana nchini Burundi chini ya uongozi wa msimamizi wa mazungumzo hayo Mzee Mkapa, wangeweza kuonesha mwanga wa maelewano kuweza kufikia muafa wa kuelekea kwenye amani.

Sisi bado tunaamini kwamba Mzee Mkapa, bado ana nafasi ya kuendelea kuzishawishi pande husika baada ya kufanya uchambuzi wa mambo waliyokubaliana na yale, ambayo hawajakubaliana katika awamu hiyo ya nne ya mazungumzio hayo kwa ujumla wake ili yakifikishwa mbele ya viongozi wa EAC, walioanzisha juhudi za mazungumzo hayo waweze kutoa mwelekeo wa nini kifuate baada ya kujitokeza hali hiyo ya mkwamo.

Tunaamini kwamba uwezekano wa kufikia muafaka upo kutokana na ukweli kwamba pande zinazohusika katika mazungumzo hayo ya mgogoro wa Burundi, zilijitokeza na kushiriki hata kama hawajafikia muafaka wowote.

Mazungumzo ya mgogoro wa kukosekana amani katika nchi fulani wakati wote siyo rahisi sana kufikiwa muafaka kwa haraka, bali uvumilivu na nia thabiti ya wahusika katika mgogoro husika kutaka kufikia mwisho na kupata suluhisho la amani, ndiyo jambo la muhimu kulisimamia.

Hapa tunapenda kutoa mwito maalumu kwa wakuu wa EAC, watakapopata taarifa rasmi kutoka kwa msimamizi wa mazungumzo hayo na kuifanyia tathmini, bila shaka watakuwa katika hali ya kutoa maelekezo na ushauri muhimu juu ya hatua zitakazoendelea kufuata katika kusaka amani ya Burundi.

Sisi tunaamini kwamba kama mgogoro wa ukosefu wa amani, uliowahi kuwepo nchini Rwanda ulishughulikiwa hadi kufikia hatua za mauaji ya kimbari na hatimaye hatua zikachukuliwa, kiasi cha kurejesha amani nchini humo, tunaamini kwamba uzoefu uliopatikana kwa suala la Rwanda, usaidie kwa kila hali kupatikana kwa suluhisho nchini Burundi.

Tunatiwa moyo kutokana na ukweli kwamba hata pande zinazovutana katika mgogoro wa Burundi, nao pia bado wana nia ya kuupatia suluhisho la amani mgogoro huo; na ndiyo sababu bado wanashiriki katika mazungumzo hayo bila kukata tamaa.