Tuongeze juhudi zaidi kukuza viwanda

SERIKALI ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli, imepania kuendesha uchumi wa viwanda, kwa lengo la kuifikisha nchi katika uchumi wa kati.

Katika mikakati ya kuelekea katika utekelezaji wa azma hiyo, serikali imeweka mkazo maalumu katika kukuza miundombinu ya usafiri wa barabara, kwa kuunganisha mikoa na miji mbalimbali na pia kujenga reli za kisasa, zitakazotumia umeme.

Ujenzi wa reli ya kisasa kwa Reli ya Kati katika kipande cha kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro umeshaanza. Ujenzi kwa kipande cha kutoka Morogoro hadi Dodoma unatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Sambamba na hayo, serikali imenunua ndege mpya mbili kwa ajili ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) na nyingine mpya ziko mbioni kuwasili hapa nchini hivi karibuni, kurahisisha usafiri wa wananchi, ikiwemo watalii kuja kufurahia vivutio vya utalii, mambo ya kale, utamaduni na mbuga mbalimbali za taifa.

Lakini, habari zilizotolewa hivi karibuni na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage juu ya kuanza kung’ara kwa sekta ya viwanda, tunayoisubiri kwa hamu, ni jambo la kutia moyo na nguvu ya aina yake.

Mwijage anasema kwa mwaka 2016, sekta ya viwanda ilitoa ajira 146,892, ikilinganishwa na ajira 139,895 zilizotolewa mwaka 2015, ikiwa ni ongezeko la asilimia 7.1. Anasema baadhi ya viwanda ambavyo vimeanzishwa katika kipindi cha mwaka 2016/17 ni vya uzalishaji chuma, saruji, vigae, nguo, mavazi, ngozi na bidhaa za ngozi.

Vingine ni vile vya kusindika nyama, vyakula, mboga, matunda, maziwa na mafuta ya kula, ambavyo vyote vina fursa kubwa ya kutoa ajira kwa Watanzania. Eneo lingine ambalo Watanzania wanatakiwa kuwekeza ni katika elimu. Baadhi ya nchi duniani, ambazo zimewekeza kwa miaka mingi katika elimu hivi leo ziko mbali.

Moja ya nchi hizo ni India, ambayo kutokana na uwekezaji wa muda mrefu katika elimu, leo hii inarusha satelaiti angani. Jambo la kutia moyo ni kuwa tayari serikali ya Rais Magufuli, imeanza kuwekeza katika elimu na inatekeleza Mpango wa Elimu Bure. Ni kweli kwamba bado hatujafikia lengo letu.

Lakini, hatuna budi kujivunia kwamba tupo katika njia sahihi ya kuelekea tunakotaka kwenda. Hivyo, kila mmoja wetu, kwa nafasi yake, bila kufanya ajizi, lazima ashiriki kikamilifu katika mikakati ya kuelekea katika uchumi wa viwanda. Tunatoa pongezi kwa serikali, kwa kuonesha mwanga wa mwelekeo wetu.

Tunaomba Watanzania wote tushirikiane katika kufikia lengo hilo la uchumi wa kati kupitia viwanda. Viongozi wa serikali, wanasiasa na wananchi, wawe tayari kutoa ushirikiano unaohitajika, kwa kuendelea kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi waje Tanzania, kuwekeza katika sekta hii ya viwanda, ambayo inaonesha kila dalili ya kuweza kuwapatia watu wetu suluhisho la tatizo la ajira.

Hakuna ubishi kwamba iwapo viwanda vitaendelea kuwekezwa nchini, vitatoa ajira na kuongeza thamani ya mazao yetu mbalimbali yatokanayo na madini, kilimo na malighafi nyingine, hivyo kupata soko na bei bora zaidi kuliko hivi sasa.

Jambo la muhimu katika mikakati hiyo ya viwanda ni kuwa tuwe tayari kutoa kila ushirikiano kwa wawekezaji, watakaoamua kuja kushirikiana nasi, bila kuwakatisha tamaa. Tunachotaka ni wawekezaji, waje wapate; na sisi wananchi, tunufaike kutokana na kuwapatia rasilimali tulizokuwa nazo wawekeze viwanda.