Meli za Mv Njombe, Ruvuma zichochee biashara

KATIKA gazeti hili jana, tulikuwa na habari ya meli za Mv Njombe na Mv Ruvuma, kufungua fursa za usafi rishaji mizigo katika Ziwa Nyasa kati ya nchi za Tanzania, Malawi na Msumbiji.

Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Benedict Mashiba aliyezipokea zilipowasili rasmi katika bandari ya Nkata Bay, Malawi, alisema ujio wake ni ufunguo wa biashara kwa nchi hizo.

Alisema usafiri wa meli hizo ni mkombozi kwa wananchi na hasa wafanyabiashara wa nchi hizo tatu, zinazotumia Ziwa Nyasa, kwani sasa ni rahisi kusafirisha mizigo mikubwa, mizito, mingi kwa wakati mmoja na kwa gharama nafuu zaidi.

Tunaungana na Balozi Mashiba, kukaribisha ujio wa usafiri wa meli hizo katika mwambao wa Ziwa Nyasa, tukiamini kuwa utaongeza ufanisi katika usafirishaji wa mizigo na bidhaa nyingine.

Tunasema utaongeza ufanisi kwa sababu usafiri wa maji unachukuliwa kuwa salama, nafuu na wa uhakika zaidi kuliko barabara. Hivyo, ujio wa meli hizo, unamaanisha biashara kati ya nchi hizo, inaelekea kuimarika na kuwa nafuu zaidi.

Kwamba, hatimaye meli hizo zimepatikana ni jambo la kuishukuru Serikali ya Tanzania, kwa kuona umuhimu wa kuimarisha usafiri wa maji katika ziwa hilo baada ya kuzorota kwa muda mrefu.

Ndio maana tunapenda kuungana na Balozi Mashiba, kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli kwa kuweka mkazo katika uimarishaji wa miundombinu ya usafiri wa meli, treni, barabara na anga pia.

Ni matarajio yetu kuwa wafanyabiashara wa nchi zote tatu, Tanzania, Malawi na Msumbiji na nyingine jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Zambia, watatumia fursa hii.

Kwa muda mrefu wafanyabiashara wa maeneo hayo, wamekuwa wakishindwa kusafirisha tani nyingine za shehena ya mizigo, wanayonunua na kusafirisha kati ya nchi hizo. Hivyo, ujio wa meli hizo, utaondoa au kumaliza tatizo hilo.

Tunaomba serikali isiishie kutengeneza meli hizo tu, bali iendelee na mpango wake wa kujenga meli za maziwa mengine kama Victoria kwa ajili ya wakazi wa Kanda ya Ziwa, utakaorahisisha safari zao majini.

Ni ukweli usiopingika kuwa usafiri wa maji ni kati ya njia nzuri na rahisi za usafirishaji mizigo, kwani ukiacha usafiri wa reli, hakuna mwingine ambao unabeba shehena kubwa za mizigo.

Itoshe tu kusema baada ya Serikali kuweka meli hizo Ziwa Nyasa, changamoto iliyobaki ni kwa wakazi wa maeneo hayo, kutumia vema fursa hiyo kujiletea maendeleo ya kijamii na kiuchumi huku wakikumbuka kuzilinda ili zidumu.

Kwa wafanyabiashara, tunaomba ujio wa meli hizo, uchochee kasi ya kufanya biashara kati yao na kuzifanya meli hizo zitumike ipasavyo na kuiingizia serikali mapato kuleta maendeleo.