Ukusanyaji wa kodi Ilala uungwe mkono na kuigw

KATIKA harakati za kuhakikisha kuwa mapato yote stahiki yanakusanywa ipasavyo na kwa wakati, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imejiwekea mikakati mbalimbali ya kuongeza wigo wa vyanzo na ukusanyaji wa mapato kikamilifu.

Katika mikakati hiyo ni pamoja na huu wa TRA kuungana na Wilaya ya Ilala katika kuhakikisha kodi ya majengo inakusanywa na hasa ikizingatiwa wilaya hiyo inakusanya kodi nyingi zaidi kuliko wilaya nyingine hapa nchini.

Hivi karibuni TRA kwa kushirikiana na uongozi wa wilaya hiyo walianza mafunzo kwa wenyeviti wa serikali za mitaa, watendaji wa kata na mitaa kuandaa mazingira ya ukusanyaji wa kodi ya majengo. Viongozi hawa walikuwa ni muhimu kwa kuwa wao ndio watu wanaokutana na wananchi moja kwa moja na mara kwa mara.

Ni dhahiri kuwa maendeleo yote ya nchi yanatokana na fedha ambayo serikali itakuwa imekusanya kutoka katika vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwa ni pamoja na kodi hizi za majengo ambako TRA na wilaya ya Ilala wanakusanya.

Kwa kukusanya kodi hizi kutasaidia kupata fedha zitakazojenga barabara, hospitali na kuboresha huduma mbalimbali kama vile maji, umeme, afya na elimu. Jambo hili ni la kupongezwa na kuigwa na halmashauri nyingine ili kuongeza zaidi wigo wa ukusanyaji mapato.

Kama ambayo Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema alisema katika semina hiyo ni kweli hakuna muujiza wowote wa fedha za maendeleo hayo kupatikana iipokuwa kuboresha ukusanyaji wa mapato na fedha zipatikane.

Viongozi wa serikali za mitaa ni watu ambao wanakutana mara kwa mara na ananchi, wanapata nafasi ya kuwaelimisha mambo mbalimbali hivyo kwa kuwashirikisha ni jambo zuri zaidi.

Mjema alisema hatawafumbia macho wenyeviti wa Serikali za Mitaa watakaokuwa kikwazo cha wananchi kulipa kodi za majengo kwa kuwa jambo hilo si la kisiasa kwa kuwa itasaidia katika kukusanya kiwango sahihi.

Na mimi naamini kabisa ni kweli suala hili sio la kisiasa hivyo liun gwe mkono na viongozi wa vyama vyote ili lifike kwa wananchi kama lilivyokusudiwa na kuleta tija. Tukisema jambo hili ni la CCM na serikali yake ni wazi halitapokewa na wananchi wote na mwisho halitaleta matokeo chanya hivyo ushirikiano ni jambo la kuzingatiwa.

Wenye viti wa mitaa nao pia wasiwe kikwazo cha wananchi kulipa kodi, watoe ushirikiano mkubwa na kuwa kiunganishi kizuri kati ya wananchi na serikali ili kuhakikisha kodi hiyo inakusanywa.

Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Kodi za Ndani, Yusuf Salum Yusuf, anasisitiza kuwa kwa sasa fedha zitakazokuwa zikikusanywa zitaerejeshwa kwa wakati ili mitaa iweze kufanya maendeleo yake.

Akasema kwa mwaka 2015/16 walikuwa na lengo la kukusanya Sh bilioni 7.82 lakini kwa mwaka huu wa fedha 2016/17 lengo lao ni kukusanya Sh bilioni 12.5, ambayo ni ongezeko la asilimia 55.

Naamini lengo hilo litafikiwa na kuvuka kama ushirikiano utakuepo na pia elimu ya kutosha itatolewa na Wenyeviti wa Serikali za mtaa kwa wananchi wao. Tusitarajie tuamke asubuhi barabara zimejengwa, zahanati zimejengwa pamoja na hospitali na pia shule zimeongezeka kama hatutatii ulipaji kodi kama ambavyo tunaelimishwa.

Katika mambo yote ambayo Rais alisema atayafanya, yanahitaji fedha na hakuna mahali pa kwenda kuzichota isipokuwa kuunga mkono hili kwa kulipa kodi mbalimbali kwa nafasi zetu.