Kila la heri Serengeti kesho

TIMU ya soka ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys, kesho itashuka dimbani kuumana na Niger kwenye michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa vijana wa umri wa miaka 17.

Inashuka dimbani kucheza mchezo huo huku ikiwa imeifunga Angola 2-1 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Stade 1 Amitie mjini Libreville, Gabon. Timu hiyo imeanza vema michuano hiyo, ambapo ilitoka suluhu na mabingwa watetezi Mali, timu ambayo ni moja kati ya timu hatari kwenye michuano hiyo.

Binafsi ninaungana na watanzania wengine katika kuitakia kila la heri timu hiyo kwenye mchezo wake huo muhimu wa kesho ambapo ni imani yangui kuwa itafanya vema. Kikubwa ambacho kimeshaonekana tangia awali ni uwezo mzuri wa wachezaji hao ambao wamekuwa wakiuonesha tangia wakiwa kambini kwenye michez yao ya kujiandaa.

Walikuwa wakipata matokeo mazuri na kushinda michezo yao ya maandalizi na kitu ambacho wanakifanya kwa sasa ni kuendeleza pale pale ambapo wameishia. Ni dhahiri kuwa wachezaji hao wameiva na wanaweza kuendeleza ushindi wao huo na kuiletea nchi sifa ambayo kimsingi imekosekana kwa muda mrefu tu.

Ni vema kwa wachezaji hao kuendelea kutambua nafasi yao katika kukata kiu ya makombe ya muda mrefu kwa watanzania na ihakikishe kuwa inatumia mwanya huu kufanikisha adhma hiyo.

Kwa upande wa watanzania tuka kazi kubwa ya kuendelea kuwaombea na kuwatakia mafanikio mema hasa kupitia viongozi walipo kwenye michuano hiyo. Kama ambavyo imekuwa wakati wa kuchangisha fedha za kuwawezesha wachezaji hao kufikia mafanikio haya ni hivyo hivyo ambavyo tunaweza kuendelea kuwasaidia wachezaji hawa.

Kwa upande wa viongozi wa timu ni vema wakaendelea kutumia nafasi zao katika kuwaelekeza wachezaji hao nini cha kufanya na nini kinachotakiwa kuepukwa wakiwa uwanjani.

Kwa kuwa Gabon wapo watanzania ambao wanaishi nchini humo ni vema nao wakajitokeza kwa wingi katika kuwashangilia wachezaji hao ili kuwaongezea hamasa. Iwapo kama wakishinda kwenye mchezo huo wa kesho basi wanakuwa kwenye mazingira mazuri zaidi ya kucheza hatua ya nusu fainali kwa kuwa watakuwa wakihitaji ushindi au sare katika mchezo wao huo dhidi ya Niger.

Binafi nina imani kubwa na timu hii kwa kuwa wachezaji hawa wanao uwezo mkubwa wa kisoka na wanaweza kuiletea heshima kubwa nchi na hivyo kilichobaki ni kuwaombea na kuwawezesha kwa kila kile kinachokuwa kikihitajika