Kutunza miundombinu ni wajibu wa kila mmoja

UJENZI wa barabara za juu jijini Dar es Salaam ni hatua nzuri itakayobadili sura ya jiji baada ya miradi hiyo iliyopo maeneo ya Tazara na Ubungo kukamilika.

Nchini Tanzania, barabara za juu hazijazoeleka, hivyo kukamilika kwa miradi hiyo kutawavutia wananchi wengi kuwa watalii kwa kuyatembelea maeneo hayo na kupiga picha kama inavyofanyika katika madaraja ya Manzese, Buguruni na yale ya mabasi ya mwendokasi yaliyopo Kimara, Ubungo Stendi ya Mkoa Ubungo pamoja na Morocco.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alipokagua ujenzi wa barabara ya juu ya Tazara takribani wiki moja iliyopita, alisema ameridhishwa na kasi ya ujenzi huo.

Ninachotaka kusema katika Wazo Langu leo ni kuwa, miradi hii ya uboreshaji wa miundombinu nchini, ni mambo mazuri ya neema yanayohitaji umakini na uzalendo ili kila mmoja awajibike kuyatunza, kuyalinda na kuyaendeleza.

Usafiri wa mabasi ya mwendokasi ulipoanza mwaka 2015, baadhi ya watu walikosea kwa kuyatumia madaraja hayo kama sehemu za kulala, na wengine kwa upuuzi, wakayatumia kama choo na sehemu ya kutupa takataka.

Hilo, likamsukuma Rais John Magufuli kuwaagiza polisi kufanya doria na kuwatia mbaroni watakaobainika kulala kwenye madaraja hayo. Kila mmoja anapaswa kutambua kuwa, miradi inayojengwa na serikali ni kwa faida ya wananchi wote hivyo, wana wajibu wa kuitunza na kuiendeleza, badala kuihujumu na kuifanyia matukio ya kinyama na kihalifu.

Kufanya hivyo, ni upuuzi sawa na kupiga ngumi ukuta huku tukijua tunaumiza mikono yetu wenyewe maana fedha zinazofanya mambo hayo ya maendeleo yetu, zinatokana na jasho letu kupitia kodi tunayotoa.

Mhandisi Miradi wa Wakala wa Barabara (Tanroads) Rajab Manger, anasema wakati inasainiwa Oktoba 2015, gharama za ujenzi wake ilikuwa Sh bilioni 88. Hizo ni pesa nyingi zinazotaka wananchi wote wenye akili timamu na matashi mema kwa taifa, wazionee uchungu na kuzitumia kwa busara na umakini.

Uharibifu unaofanywa na baadhi ya watu hata katika barabara za mabasi ya mwendo kasi jijini Dar es Salaam, unaleta mtazamo hasi na unaopotosha kwamba, miradi ya serikali siyo yetu wananchi.

Hii ndiyo inayowafanya wengine kuiharibu au kuitumia vibaya kwa makusudi miradi inayoendeshwa na serikali bila kujua kuwa, wanapiga ngumi ukuta kuumiza mikono yao.

Kimsingi, hata waungwana wasioiharibu miundombinu na miradi mingine inayojengwa na kutekelezwa na serikali, baadhi wanakosea kuona kuwa siyo wajibu wao kuzuia uharibifu huo, au kuutolea taarifa kwa vyombo husika ili wahusika hao wachukuliwe hatua za kisheria.