Kampuni nyingine nazo zidhamini ligi nchini

HUKU Agosti 26 mwaka huu ndio pazia la msimu wa Ligi Kuu likifunguliwa, kuna haja kwa kampuni mbalimbali kujitokeza kudhamini ligi hiyo. Kwa sasa Ligi Kuu Tanzania bara ina wadhamini kadhaa huku mdhamini mkuu akiwa ni Vodacom, lakini kuna haja ya kampuni nyingine zaidi kujitokeza.

Hiyo itasaidia kuinua kiwango cha wachezaji kwa kuwa klabu zao zitakuwa na fedha nyingi ambazo inaweza kuzitumia katika kuwalipa wachezaji mishahara mizuri. Lakini itasaidia kuimarisha zaidi Ligi kwa kuwa klabu zitakuwa na fedha za kutosha kumudu gharama mbalimbali za kuendeleza timu zao.

Suala la usafi ri, huduma za maradhi na mengineo muhimu katika kuwaendeleza wachezaji ambao ndio kiungo kikuu kwenye Ligi. Ni dhahiri kuwa Ligi Kuu Tanzania bara ina wapenzi wengi na huku wengine wakiwa wenye kuifuatilia mwanzo hadi mwisho wake na hii ni ishara kuwa hata kampuni zikijitangaza kupitia ligi hiyo basi zitakuwa zimejiweka mazingira mazuri zaidi ya kukuza biashara zao.

Udhamini huo sio tu unahitajika kwenye Ligi Kuu peke yake bali hata pia kwenye Ligi za Daraja la Kwanza hasa timu za mikoani ambapo kuna vipaji vingi. Iwapo kama uwekezaji ukifanywa kuanzia huko itasaidia kwa kiasi kikubwa kuibua vipaji ambavyo vitakuja kusaidia timu za Ligi Kuu. Wakati hayo yakitakiwa kufanyika ni vema kwa sasa klabu kuhakikisha kuwa na zenyewe zinajitambua kwa kuweka masharti mwafaka ya udhamini huo.

Kumbukeni kuwa udhamini wa kampuni kwa klabu zenu ni suala linalopaswa kuhakikisha kuwa kila pande inanufaika nayo na sio upande mmoja. Kwa timu za Ligi Kuu zitambue kuwa thamani ya timu zao kushiriki Ligi Kuu hilo peke yake lina upekee na ni la thamani kwa klabu zao sasa kampuni inapoingia makubaliano ya kudhamini timu zao basi kuwe na uwazi na ufanisi utakaosaidia kukuza pande zote.

Klabu zitambue thamani zao hasa ikizingatiwa kuwa kwa ushiriki tu kwenye ligi hiyo klabu zinaonekana ndani na nje ya nchi kupitia luninga na hivyo kampuni zikijitangaza nazo zitajulikana kupitia timu hizo, sasa kuna haja ya kuomba udhamini uwe mkubwa