Uzalendo unahitajika kwa vijana watakaosomea gesi na mafuta

NI jambo la faraja kuona wanafunzi 22 kutoka nchini, kuchaguliwa kwenda nchini China kwa ajili ya kusomea fani za utafi ti na uchimbaji mafuta na gesi, ambapo inaongeza idadi na kufi kia 82.

Hatua hii ni kubwa kwa kuwa Taifa ambalo limewaamini vijana hao kwamba watakuwa wataalamu bora wa baadaye watakaoisaidia Tanzania kufikia malengo yake hususani katika masuala ya mafuta na gesi.

Naamini kuwa idadi hii ni ishara ya kukua kwa sekta ya mafuta na gesi nchini na kwamba itasaidia Tanzania kuwa na wataalamu wengi kwenye sekta hiyo ya mafuta na gesi, kwa kuwa tayari ipo miradi mbalimbali ambayo kama nchi imeanza kuifanya inayohitaji wataalamu.

Kutokana na ugunduzi wa gesi asilia na mafuta hapa nchini, vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa, wanahitajika kwa wingi kwa ajili ya kuonesha utaalamu wao wa namna ya kushauri, kutafiti na kuboresha sekta hiyo.

Vijana hao wanapaswa kutambua kwamba uzalendo ndiyo msingi wa maendeleo ya nchi, hivyo wahakikishe kuwa mara baada ya masomo yao, waweze kuitumikia Tanzania ipasavyo katika sekta hiyo muhimu kwa ukuaji wa uchumi.

Mara nyingi vijana wanapopata fursa kama hizo, wanaangalia zaidi kufanya kazi katika nchi nyingine na kusahau kwamba serikali inafanya jitihada kuhakikisha kwamba vijana wenye sifa, wanakwenda kusoma nje ya nchi kwa kutumia kodi za wananchi.

Wahenga walisema ‘Mkataa kwao ni Mtumwa’ kwa hiyo vijana hawa wanapaswa kuishi msemo huu, ambao lengo lake ni kusisitiza uzalendo na wafanye kila wanaloweza, kuhakikisha wanasoma kwa bidii na kuonesha kwa vitendo ni kwa namna gani tutaweza kufanikiwa katika sekta ya mafuta na gesi.

Natambua kuwa wapo wanafunzi wengi wanaodhani kwamba kusoma nje ya nchi na kufanya kazi huko ndiyo ufahari, la hasha, kwani itakuwa ni jambo la aibu kuona wasomi kama hao wanaendeleza nchi za watu huku wakiiacha Tanzania ikijikongoja.

Kila mmoja anapaswa kuona uchungu na nchi yake kwa kuhakikisha kuwa anasimama kidete kuleta maendeleo ya nchi, kwa kutumia utaalamu walionao na siyo kuelekeza kwa kupitia mitandao ya kijamii, ikiwa uwezo wa kurudi na kufanya kazi kwa vitendo wanao.

Aidha, nitumie fursa hii kuipongeza serikali ya China ambayo imedhamini mafunzo hayo kwa miaka mitano, ambapo kwa sasa ni miaka minne ambayo kila mwaka wanafunzi 20 wanakwenda kusoma nchini China.

Ushirikiano huu unapaswa kudumishwa kwani unasaidia kuongeza idadi ya wataalamu katika sekta mbalimbali, hivyo wanapaswa kuungwa mkono katika jitihada zao za kuisaidia serikali. Ni rai yangu kwamba vijana hawa, wataungana na serikali kuhamasisha vijana wenzao waliotangulia, kujenga tabia ya kuwa wazalendo kwa kuipenda nchi yao na kuisaidia pindi itakapowahitaji.