NGOs zitumie vizuri muda wa nyongeza

JUZI serikali ilitangaza kuongeza muda wa uhakiki wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini (NGOs) ili kuyawezesha mashirika mengi zaidi kupata nafasi ya kuhakikiwa kuhusu uendeshaji wa shughuli zao.

Serikali imeongeza zaidi ya wiki mbili kutoka tarehe ya mwisho iliyokuwa imepangwa awali ya Septemba 4, hadi kufikia Septemba 20, mwaka huu. Uamuzi huo wa busara wa serikali ulitangazwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Sihaba Nkinga.

Kiongozi huyo wa serikali alisema kimsingi serikali imeona kuna ulazima wa kuongeza muda huo ili kukamilisha uhakiki wa NGOs zaidi ya 8,316 zilipo nchini. Naungana na Katibu Mkuu katika kuwahimiza wadau wote wa mashirika haya muhimu katika mipango maendeleo, kujitokeza kutumia muda ulioongezwa ili kuhakikiwa.

Hii ni kwa kuwa kama ilivyosema Serikali, kwa muda wa awali ni wazi mashirika mengi yalikuwa hayajitokeza ili kuhakikiwa. Ingawa taarifa ya serikali ilionesha baadhi ya kanda kufanya vizuri, lakini kanda nyingine ambazo mikoa yake imeonekana kuwa na mwamko mdogo wa kujitokeza ili kuhakikiwa na ni imani yangu kuwa sasa watajitokeza.

Tofauti na hilo, nitakuwa miongoni mwa Watanzania ambao tutawashangaa wamiliki au waendeshaji wa NGOs watakaojitokeza na kuilaumu serikali mashirika yao yatafutwa kutokana na kukiuka agizo hilo la serikali.

Naamini mashirika yatakayojitokeza sasa yatazingatia maelekezo sahihi yaliyotolewa na serikali ikiwemo kuwa na stakabadhi sahihi za malipo na zitawatumia mawakala waaminifu. Inaqshangaza kusikia kuwa, mbali ya baadhi ya stakabadhi kutokuwa sahihi pia uhakiki umebaini kuwapo mashirika ambayo hayajawahi kutoa ada ya mwaka hata mara moja.

Hata hivyo napongeza kwa dhati hatua ya wizara kuwataka wahusika wafike kuhakikiwa wasiogope suala la kudaiwa ada hizo. Hii ni nafasi muhimu kuitumia vema. Kwa namna yoyote ile, endapo kutakuwa na mashirika yatakayoshindwa kujitokeza hata baada ya muda kuongezwa, tutalazimika kuamini kuwa wahusika wa mashirika hayo wanaendesha shughuli haramu na hivyo wameamua kujificha.