Elimu ya juu tumieni vizuri muda wa mkopo ulioongezwa

MWISHONI mwa wiki, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) ilitangaza kuongeza muda wa siku saba kwa wanafunzi waombaji mkopo ili waweze kukamilisha taratibu zote za uombaji na kuweza kuhakikiwa kama wamekidhi vigezo vya kupata fedha hizo kwa ajili ya masomo ya elimu ya juu.

Bodi iliongeza muda huo ikiwa ni kuwezesha kila mmoja mwenye sifa za kupata mkopo huo aweze kuupata na kuendelea na masomo ya elimu ya juu yatakayowezesha kutimiza ndoto zao.

Awali kabla ya Bodi kuongeza muda huo, dirisha la wanafunzi hao kuomba mkopo lilitarajiwa kufungwa leo, lakini kwa kuona ipo haja ya walio wengi kushiriki kwa kuomba mkopo utakaowawezesha kusoma masomo yao ya elimu ya juu ndipo walipoongeza muda.

Kufunguliwa kwa dirisha la wanafunzi kuomba mikopo kutawezesha wanafunzi 30,000 wa mwaka wa kwanza wa masomo kwa 2017/18 kupata mikopo ya elimu ya juu huku wanafunzi 93,292 wakiwa wanaendelea kupokea mikopo hiyo kwa ajili ya kukamilisha masomo yao.

Akizungumza juu ya kuongezwa kwa muda huo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru anasema Bodi hiyo imetenga jumla ya Sh bilioni 427 kwa mikopo yote ikiwa ni kwa ajili ya wanafunzi wapya na wale ambao awanaendelea na masomo katika ngazi mbalimbali.

Anasema hadi kufikia mwishoni mwa wiki, jumla ya waombaji wa mikopo kwa njia ya mtandao walikuwa 49,282, kati yao waombaji 15,473 wakiwa wamekamilisha maombi yao kwa njia ya mtandao kwa kufuata taratibu zote za uombaji zilizotolewa na Bodi.

Kutokana na kuongezwa kwa muda na Bodi hiyo, ni wakati sasa kwa wanafunzi wanaotarajia kuomba mikopo kuhakikisha wanatumia vyema muda huo na kukamilisha taratibu zote zilizowekwa ili waweze kupata mkopo kwa mujibu wa vigezo vinavyotakiwa.

Haitarajiwi kuwa kwa muda ulioongezwa wapo wanafunzi wanaohitaji mkopo kwa ajili ya kuendelea na masomo yao ya elimu ya juu, watakaoshindwa kutekeleza masharti yanayohitajika ili kukamilika kwa maombi yao na mwishio wa siku wabaki wakilalamika kwa kukosa fursa hiyo.

Aidha, pamoja na kuongezwa kwa muda huo, pia ili kuhakikisha kuwa wahitaji hawatokosa mkopo huo, ni muhimu kwa kila mmoja kuweza kusoma kwa makini masharti na vigezo vinavyotakiwa kutekelezwa wakati wa kujaza fomu hizo na kujua ni wapi wanapotakiwa kuziwasilisha.

Kwa maana hiyo, endapo watakuwepo wanafunzi ambao hawatokidhi masharti ya kujaza fomu hizo na namna ya kuziwasilisha kwa Bodi kama inavyotakiwa ni wazi kuwa watakuwa ndiyo chanzo cha kuwepo kwa malalamiko juu ya mfumo wa uombaji wa mikopo.