Kongamano la Kiswahili lisaidie kukuza Kiswahili EAC

KONGAMANO la kwanza la Kiswahili, lililoandaliwa na Jumuiya Afrika Mashariki (EAC), linatarajiwa kufanyika Septemba 6 hadi 7.

Kongamano hilo litawashirikisha wajumbe zaidi ya 150 kutoka sehemu mbalimbal za ndani na nje ya Afrika Mashariki. Mbali ya Tanzania, washiriki wengine wanatoka Burundi, Rwanda, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Senegal, Namibia na Uturuki.

Kaulimbiu ya kongamano hilo ni ‘Kuleta Mabadiliko katika Jumuia ya Afrika Mashariki kupitia Kiswahili’ huku lengo la kongamano hilo likiwa ni kuleta umoja na mshikamano na kuhakikisha Kiswahili kinakua.

Ni matumaini yangu kuwa kufanyika kwa kongamano hilo, kutasaidia kuleta ushirikiano na kujadili mambo mbalimbali yatayoweza kukuza na kuiendeleza lugha ya Kiswahili hasa katika nchi zilizo katika jumuia ya Afrika Mashariki.

Ni wazi kuwa lugha hiyo ni rasilimali, hasa kwa sasa baada ya nchi nyingi Afrika, kuitambua huku nyingine ikipitisha lugha ya Kiswahili, kuanza kutumika rasmi kama moja ya lugha kuu ya mawasiliano katika nchi zao.

Kwa Tanzania ambao ndiyo waasisi wa lugha hii, ni nafasi yetu sasa kusimama imara na kuhakikisha tunatumia fursa hii kukitangaza Kiswahili na kuangalia fursa zilizopo katika kukieneza.

Pamoja na kwamba nchi nyingine zinatumia Kiswahili, lakini kwa Tanzania tunayo nafasi nzuri zaidi, tuna walimu wa kutosha ambao kama watawezeshwa kutumika kufundisha, itasaidia siyo tu kukuza Kiswahili lakini pia kufungua fursa nyingine ya ajira.

Ni wakati mzuri Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) kufanyia kazi ushauri wa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kuwa na mfumo ambao utawatambua walimu wote wa Kiswahili waliopo nchini ili watakapohitajika iwe rahisi kupatikana.

Natumaini pia kuwa mkutano huu pamoja na mambo mengine, utasaidia kuelezea umuhimu wa kutumia lugha hiyo kwa mawasiliano baina ya wananchi wa nchi za jumuia hiyo, kwani kuna baadhi ya watu hawaamini kuwa Kiswahili kina mchango mkubwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa Kamisheni ya Kiswahili, tayari imeanza kukitangaza Kiswahili. Hili ni jambo jema, kwani tayari imeanzisha mpango wa kustawisha na kuendeleza Kiswahili ili kuondoa changamoto kwa wale wasiofahamu lugha hiyo.

Aidha, wanahabari ni wadau wakubwa na wana mchango muhimu katika kuchangia maendeleo ya Kiswahili katika ukanda wa Afrika Mashariki na dunia, kwa kukitangaza na pia kutumika kufundisha.

Kwa upande wake, Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) kwa kutumia gazeti la HabariLeo, inafundisha Kiswahili katika Ukanda wa Afrika Mashariki, kupitia mpango maalumu wa kukuza Kiswahili.

Hii ni fursa pia kwa waandishi wa vitabu, kuandika vitabu vya kutosha vya kujifunzia Kiswahili ambavyo vitauzwa katika nchi za Afrika Mashariki kwa ujumla, ambavyo vitasaidia mtu mmoja mmoja kujifunza.

Pamoja na jitihada hizo, viongozi wetu wa nchi pia katika kukuza lugha ya Kiswahili, wana wajibu wa kuitangaza lugha ya Kiswahili kwa kuitumia katika mikutano mbalimbali ya kitaifa na hata kitaifa tena kwa fahari kubwa.

Katika hili nampongeza Rais wa sasa, Dk John Magufuli kwa kuwa mstari wa mbele katika kukuza Kiswahili, kwani katika mikutano yake anapokutana na viongozi wa nchi nyingine, amekuwa akitumia lugha ya Kiswahili