Wanawake zingatieni aliyosema Makamu wa Rais

TAMASHA la W a n a w a k e 2017 lililoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania, (TGNP) limefungwa juzi ambapo wanawake kutokea mikoa mbalimbali walihudhuria.

Tamasha hilo lilifunguliwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan aliyetoa mwito kwa wanawake na wadau wengine wanaopambania haki, ulinzi na usalama wa wanawake nchini.

Alitoa mwito kwa wanawake kuwa makini katika kutumia fedha za mikopo wanazokopeshwa katika kuendeleza miradi yao, badala ya kununulia mavazi na mapambo na kufanyia sherehe.

Makamu wa Rais aliwahimiza wanawake kutoficha fedha zao kwenye kabati, badala yake, waziingize kwenye mzunguko wa kibiashara au kuziweka benki. Kimsingi, wanawake wazingatie kufika walipokusudia wanapoanzisha miradi kwa kuepuka vishawishi na uzembe unaowaweka baadhi katika mazingira mabaya na kuiona mikopo kuwa tatizo, badala ya ukombozi.

Wanawake wajenge utamaduni wa kuheshimu na kutofautisha mali za miradi (biashara) na mali zao binafsi kwa ajili ya matumizi. Nidhamu hii ikizingatiwa, wataiona faida ya mikopo katika miradi.

Wakizingatia hilo, ni wazi watatimiza ndoto zao katika kujikwamua dhidi ya umaskini na hatimaye kustawisha uchumi wa familia zao na taifa kwa jumla. Wazingatie ushauri wa makamu wa Rais wa kujenga utamaduni wa kuinuana wenyewe kwa wenyewe kwanza hasa katika masuala yaliyo ndani ya uwezo wao katika nyanja za siasa, elimu, teknolojia, ujasiriamali na hata michezo na sanaa.

Kwa kuzingatia ushauri wa Mama Samia, wanawake wazingatie kuwa, mkombozi wa mwanamke kabla hajapata nguvu na kuungwa mkono na upande wa pili, ni mwanamke mwenyewe.

Huu ni wakati kwa wanawake kugeuka na kukataa kasumba ya kukwamishana au kurudishana nyuma, badala yake, wanyanyuane kwa manufaa yao na familia zao, na hata taifa kwa jumla.