Uchaguzi wa marudio Kenya uwe wa amani

UCHAGUZI wa marudio nchini Kenya unatarajiwa kufanyika Oktoba 17, mwaka huu baada ya ule wa awali kutenguliwa na mahakama ya juu ya nchi hiyo kutokana na dosari zilizojitokeza.

Mahakama ilitengua ushindi wa Kenyatta wa Chama cha Jubilee ambaye awali alitangazwa kushindwa kwa kura milioni 8.2 sawa na asilimia 54.27, ikiwa ni baada ya mpinzani wake Muungano wa Vyama vya Upinzani (NASA), Raila Odinga aliyepata kura milioni 6.7 sawa na asilimia 44.74, kupinga ushindi huo mahakamani.

Kutokana na uamuzi wa mahakama wa kutaka uchaguzi wa nafasi ya urais kurudiwa, tayari Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya (IEBC), Wafula Chebukati amebainisha kuwa hakutakuwa na uteuzi mpya wa wagombea wa urais.

Pia alisema kuwa marudio hayo yatahusisha wagombea wa vyama viwili pekee, yaani Kenyatta na mgombea mwenza, William Rutto wa Jubilee na Odinga na mpinzani mwenza, Kalonzo Musyoka kupitia muungano wa NASA.

Kutokana na kurudiwa uchaguzi katika ngazi ya urais na kushirikisha vyama viwili peeke ni vema Wakenya wakaendeleza hali ya amani na utulivu ili kusitokee uharibifu wa aina yoyote.

Wakumbuke kuwa katika mashindano ya aina yoyote kuna kushinda na kushindwa, maana yake ni kwamba uchaguzi wa marudio utakapofanyika na matoleo kuwekwa hadharani wakubaliane nayo pasipo vurugu na endapo watakuwa na wasiwasi nayo badala ya kufanya vurugu waende kwenye vyombo vinavyohusika kwani hiyo ndiyo demokrasia inayotakiwa.

Katika uchaguzi wa marudio ni vema pande zote za Jubilee na ule wa NASA kuhakikisha amani inakuwepo ili Wakenya na wageni kutoka nchi nyingine wawe katika hali ya usalama.

Hali ya utulivu itawafanya wazee, wagonjwa, watoto pamoja na wamama wanaotunza familia kufanya shughuli zao za kawaida kwa amani pasipo kubughudhiwa kwa namna yoyote ile.

Pia itawawezesha wafanyakazi kwenda kazini kwao, wafanyabiashara katika shughuli zao na wanafunzi kwenye masomo yao pasipo kuwa na wasiwasi wa kuumizwa kwa kuwa amani itakuwepo.

Wakenya wanatakiwa kutambua kuwa vurugu si njia ya kutatua matatizo yoyote yatakayojitokeza wakati wa uchaguzi wa marudio na badala yake itakuwa ni kuharibu nchi ambayo wamepewa na Mungu.

Siku zote vurugu zinarudisha maendeleo ya nchi na wananchi wake kwani, hata siku moja vurungu haziwezi kuwafanya wananchi kuzalisha mali kwa ajili yao na familia zao na taifa kwa ujumla.

Vurugu hazihatarishi Wakenya na nchi ya Kenya pekee, bali hata nchi jirani kama Tanzania, Uganda, Rwanda na Burundi zitaingia kwenye usumbufu na hali ya usalama kuwa shakani.

Siku zote nchi ikiwa na vurugu na kukosa utulivu na amani katika nchi, inakuwa fursa ya wabaya na wakwapuaji wa rasilimali za nchi kutumia fursa hiyo kujinufaisha huku wananchi wakihangaika.

Ni wakati sasa wa viongozi wa dini kutoka maeneo mbalimbali ya Afrika Mashariki na Kenya yenyewe kuihubiri amani katika nyumba zao za ibada. Pia viongozi wanaogombea nafasi hiyo kutumia mikutano ya kuzungumza na wafuasi wao kusisitiza suala zima la amani. Agenda yao pamoja na kuomba kura iwe ni kusisitiza amani. Shime raia wa nchi jirani tuungane na Wakenya kuomba amani.