Watani wa jadi onesheni uhenga katika soka nchini

NI pambano la kukata na shoka leo wakati Yanga na Simba watakaposhuka dimbani kucheza katika mchezo wao wa kwanza katika msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Timu hizo, ambazo zinalingana kwa pointi huku kila moja ikiwa na 15, lakini zinatofautiana kwa mabao tu, hadi sasa zinaonekana kuwa na nguvu sawa. Katika mechi zao za mwizho, Simba ilishinda mabao 4-0 dhidi ya timu iliyopanda daraja ya Njombe Mji wakati watani wao Yanga wenyewe nao walipata ushindi kama huo walipocheza ugenini dhidi ya Stand United.

Hilo tu la timu hizo kila moja kupata ushindi mnono kunaongeza hamasa kuwa timu hizo kwa sasa ziko vizuri na yeyote anaweza kushinda. Pia kwa timu hizo kila moja kushinda tena kwa idadi ya mabao inayolingana na mwenzake, hilo linawafanya mashabiki wa timu hizo washindwe kutambiana kuwa mwenzake ni mkali kuliko mwingine.

Lakini pamoja na timu hizo kuonekana kama zikilingana kwa kila kitu, lakini zinapokutana zenyewe kwa zenyewe zinacheza mchezo ambao haueleweki. Mara nyingi mashabiki wameshindwa kupata kile wanachotarajia timu hizo zinapokutana kwani zimekuwa zikicheza soka bovu, ambalo halima mvuto kabisa.

Ni matarajio ya safu hii kuwa Yanga na Simba leo zitacheza soka safi , ambalo litakuwa kivutio kikubwa kwa wapenzi wa soka watakaofi ka Uwanja wa Uhuru kulishuhudia au wale watakaokosa tiketi watakapokuwa mbele ya TV zao au katika vibanda umiza.

Timu hizo zinaweza kucheza soka safi kama zikiondoa mchecheto na kukamiana kwani zina wachezaji wazuri na wenye uwezo mkubwa. Watu wanakwenda uwanjani ili kuona soka safi na ushindi na sio kwenda kuangalia mambo ya imani za kishirikina, ambapo timu zinashindana kutupa hirizi na kufukia vitu golini au katikati ya uwanja.

Yanga na Simba ni timu kongwe na zina umri wa zaidi ya miaka 50, lakini zimeshindwa kuonesha ukongwe wao katika soka la nyumbani na hata lile la kimataifa kwa kushindwa kufanya vizuri, ebu onesheni ukongwe wenu basi kama soka.

Mbali na kuwa na wachezaji wazuri, pia timu hizo zina makocha bora ambao wana uwezo mkubwa wa kufundisha na kupata matokeo mazuri kwa timu zao. Napenda kuwakumbusha Yanga na Simba kucheza soka safi ili kutoa burudani kwa wapenzi wa soka watakaotoa fedha zao, Sh 10,000 na 20,000 ili kuliona pambano hilo