Viongozi wa michezo wajifunze kutoka TOC

MKUTANO Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) utafanyika mjini Zanzibar, Desemba 10 mwaka huu.

Tayari maandalizi ya mkutano huo yameanza, ikiwamo mialiko kutumwa kwa viongozi wa vyama au mashirikisho ya michezo nchini. Kila chama au shirikisho la michezo hutoa mwakilishi mmoja kwa ajili ya kuhudhuria mkutano huo mkuu, ambao hufanyika kwa kupokezana kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Mwaka juzi mkutano huo ulifanyikia Zanzibar na mwaka jana Tanzania Bara na sasa mwaka huu ni zamu ya visiwani kuuandaa. TOC imekuwa ikitekeleza katiba yake kwa kuendesha mkutano huo kila mwaka bila kukosa na sio tu kuuandaa pia imekuwa ikisoma taarifa ya mwaka ya fedha, ya maendeleo na mambo mengine tofauti na vyama vingine.

Vyama vingi vya michezo vimeshindwa kuandaa mikutano yao mikuu kwa wakati na hata vingine vinapofanya hujaa ubabaishaji katika uendeshaji wake. Viongozi wa michezo watakaohudhuria mkutano huo mkuu wajitahidi kujifunza vitu kutoka TOC kuanzia uendeshaji wake na mipangilio mingine.

Mbali na viongozi wa vyama na mashirikisho ya michezo kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, pia mkutano huo huhudhuriwa na viongozi wa michezo wa serikali zote mbili za Tanzania na Zanzibar.

Mfano wakurugenzi wote wa michezo wa pande mbili wamekuwa wakialikwa, makatibu wa mabaraza yote mawili na wengine wamekuwa wakialikwa na kutoa mawazo yao pale inapobidi.

Hakuna ubishi kuwa TOC ni moja ya taasisi za michezo, ambazo zimekuwa zikiendesha shughuli zake kwa utaratibu mzuri unaoeleweka. Na hilo limekuwa likidhihirika wakati wa mikutano yao mikuu, ambayo imekuwa ikifanyika kila mwaka.

Taasisi hiyo imekuwa na utaratibu mzuri kuanzia utoaji wa makabrasha, kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu, uandaaji wa mahali pakufi kia na mambo mengine. Hatahivyo, pamoja na wajumbe kuyaona mazuri hayo, lakini wameshindwa kabisa kwenda kuyatekeleza katika vyama au mashirikisho yao ya michezo. Ubabaishaji ndio kitu cha kwanza, ambacho kinasababisha viongozi kushindwa kuiga yanayofanywa na TOC.