Tuchunge watoto shule

MUHULA mpya wa masomo shule za msingi na sekondari nchini unatarajiwa kuanza kesho nchini kwa shule nyingi kufunguliwa baada ya kufungwa kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka, sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.

Kufunguliwa kwa shule hizo kunatoa fursa ya wazazi na walimu kubeba majukumu mapya ya utekelezaji sera ya elimu inayomtaka kila mzazi kumpatia elimu mtoto, walimu kutimiza wajibu wao kwa kufundisha kwa ufasaha wakati wote.

Mwanzo wa mwaka wanafunzi hupanda kutoka darasa moja kwenda lingine baada ya kupitia hatua fulani katika mwaka mzima wa masomo. Mathalani wapo wanaotoka darasa la awali hadi la kwanza, darasa la saba hadi kidato cha kwanza na kuendelea katika ngazi nyingine.

Hiki ni kipindi ambacho wazazi wengi ‘vichwa’ vyao huwaka moto kutokana na majukumu makubwa ya kuhakikisha mahitaji yote kwa ajili ya mwanafunzi kwenda shule yanapatikana.

Mahitaji hayo ni kuanzia sare, madaftari ada ambapo kwa baadhi ya shule hasa za binafsi kwa kiasi kikubwa suala hilo huwa pasua kichwa kutokana na kuhitaji fedha za kutosha. Changamoto inayojitokeza kipindi hiki ni pale ambapo watoto wadogo hususani wanaoanza darasa la kwanza, wanapokosa uangalizi maalumu kutoka kwa jamii, wazazi na walezi.

Hawa hukosa uangalizi wanapokwenda au kutoka shule na kujikuta wakihatarisha maisha yao kutokana na uwepo wa wingi wa vyombo vya usafiri na madereva wasiozingatia sheria.

Ikumbukwe watoto wengi wanaoanza darasa la kwanza zaidi hutokea mijini huku bado akili zao zikiwa hazina upeo mkubwa wa kukabiliana na ‘vurugu’ za barabarani na hivyo kutumia muda mwingi kushangaa au kucheza barabarani pindi watokapo au kwenda shuleni na kuwa hatarini.

Kuna ajali mbalimbali zilizowahi kuripotiwa nchini kipindi cha nyuma zikihusisha watoto wadogo wanaoanza shule wapitapo barabarani. Kama jambo hili halitafanyiwa kazi katika nyakati hizi, madhara yake yanaweza kuendelea kujitokeza siku za usoni na kutuachia majonzi.

Napenda kuiasa jamii nzima hususani wazazi kuhakikisha wanatekeleza ipasavyo majukumu yao, waweke utaratibu mzuri kulinda watoto shule kwa kuwavusha salama wanapovuka barabara kwa ku ajali.