Mvua zitumike kuongeza uzalishaji wa mazao EAC

MSIMU wa mvua umeanza katika maeneo mengi kwenye nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mvua hizi ni muhimu kwa shughuli za kilimo cha mazao mbalimbali yakiwemo ya chakula na biashara.

Tunatambua kwamba, baadhi ya nchi wanachama wa Afrika Mashariki zilikabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula kutokana na ukosefu wa mvua uliosababisha kuwepo kwa ukame kwenye baadhi ya maeneo.

Upungufu huo wa chakula, umekuwa ukiwalazimu wafanyabiashara kusafiri hadi nchi nyingine wanachama wa Jumuiya hiyo kununua nafaka ili kuokoa maisha ya watu kwenye nchi zao.

Kwa mfano hivi karibuni imeripotiwa kwenye vyombo vya habari kwamba, wafanyabiashara wa nafaka kutoka Tanzania, Kenya na Rwanda walikimbilia nchini Uganda kununua mahindi ya bei nafuu.

Ikilinganishwa na nchi nyingine wanachama, hali ya mavuno ya nafaka nchini Uganda ilielezwa kuwa nzuri wakati maeneo mengine ya ukanda huu yakikumbwa na ukame. Katika msimu uliopita, taarifa zinasema kuwa Uganda iliuza takribani tani 38,000 za mahindi kwa nchi jirani yenye thamani ya dola milioni 15.2, huku kiasi kikubwa cha tani 30,500 kikiuzwa nchini Kenya.

Mbali na Kenya, Rwanda kupitia vituo vyake vya mipakani vya Gatuna na Cyanika viliingiza tani 5,405 ya nafaka kutoka Uganda kwa kipindi hicho hicho, ikifuatiwa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambayo iliagiza tani 1,105 kupitia vituo vya mipakani vya Rusizi, Mpondwe na Rubavu, huku Tanzania ikiagiza tani 480 kupitia mpaka wa Mutukula.

Kutokana na uhitaji mkubwa wa chakula miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, natoa wito kwa mamlaka husika za kilimo kuwahamasisha wananchi kuzitumi vyema mvua zinazonyesha kwa kuzalisha mazao ya chakula.

Ukanda wa Afrika Mashariki ni miongoni mwa maeneo machache duniani ambako sehemu kubwa ya ardhi yake bado ina rutuba ya kutosha licha ya changamoto ya uhaba wa mvua kwa baadhi ya nyakati.

Kinachotakiwa ni Serikali za Jumuiya hiyo kupitia wizara zao za kilimo na maofisa ugani kutoa elimu na hamasa kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia mvua zilizopo kwa kulima mazao ya muda mfupi ya chakula ili kukabiliana na baa la njaa.

Chakula ni moja ya mambo ya msingi yanayoleta siyo tu utulivu kwa nchi, bali pia heshima kwa utu wa watu wake. Hivyo basi, licha ya kuwa tuna fursa ya kuuziana chakula kama nchi wanachama, lakini pia ni vyema kila serikali ya taifa mwanachama inachukua hatua za makusudi za kuhakikisha wananchi wake wanazalisha chakula cha kutosha, pamoja na kuwapatia mahitaji ya msingi kama vile pembejeo na ushauri wa kitaalamu