Viongozi wa BFT mmesahau nini katika ofisi zenu?

UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Ndondi Tanzania (BFT) umepangwa kufanyika Februaria 25 mjini Dodoma ambako viongozi wapya watachaguliwa.

Viongozi wa BFT kama yalivyo mashirikisho au vyama vingine vya michezo ambavyo michezo yao ni ile ya Olimpiki, wamekuwa wakikaa madarakani kwa kipindi cha miaka minne tangu walipochaguliwa.

Tayari Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limeanza kutoa fomu kwa ajili ya wadau wenye sifa wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali katika shirikisho hilo la ndondi (BFT) Tanzania. Baadhi ya viongozi wanaomaliza muda wao akiwemo rais na katibu wake mkuu, Rutta Rwakatale pamoja na Makore Mashaga tayari wamechukua fumu kutaka kuendelea kuongoza shirikisho hilo.

Rwakatale amechukua tena fomu kutaka kutetea nafasi yake hiyo ya urais wakati Mashaga yeye ameona kwa sasa angalau apande juu kwa kuchukua fomu ya umakamu uenyekiti.

Viongozi hao wameongoza BFT kwa miaka minne na miezi kadhaa sasa tangu walipoingia madarakani katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Bagamoyo, lakini Rwakatale yeye aliingia miezi kadhaa baadae katika uchaguzi mdogo uliofanyika jijini Dar es Salaam baada ya ule wa Bagamoyo kushindwa kumpata rais.

Sasa ngoja nizungumzie uchaguzi ujao utakaofanyika Februari 25, 2018 kwani kuna mambo kadhaa yananishangaza, hasa pale kuona baadhi ya viongozi waliopita eti wanataka kuongoza tena.

Uongozi uliopita pamoja na ni haki yao ya kikatiba kugombea na hata kuongoza tena, lakini mimi sikubaliani nalo na nitawashangaa sana wajumbe kama watawachagua tena. Wajumbe wa Mkutano Mkuu ndio wenye jukumu la kuchagua viongozi wao watakaokaa madarakani kwa miaka minne baada ya majina yao kupitishwa na wasimamizi wa uchaguzi huo, BMT.

Mbali na kuwashangaa wajumbe kama watawarudisha tena viongozi hao, pia nitawashangaa zaidi BMT kama nao watawapitisha viongozi hao katika mchujo wao. Nasema nitashangaa kwa sababu, kwa upande wangu sioni walichofanya cha maana hasa kimataifa katika kuuendeleza mchezo huo ambao huko nyuma Tanzania ilikuwa ikijivunia kwa mabondia wake kufanya vizuri kimataifa.

Nadiriki kusema kuwa BFT hata kitaifa tu haikufanya vizuri kwani walishindwa kuendesha mkutano mkuu kwa miaka kadhaa baada ya akidi kutotimia, yaani wajumbe wa mkutano mkuu walishindwa kufi kia idadi inayotakiwa.

Hilo tu ni aibu kubwa, kwani uongozi ulishindwaje kutoa taarifa mapema kwa wajumbe wao wa mikoa hadi kushindwa kufi kia idadi inayotakiwa? Kukosekana kwa wajumbe hao kulisababisha kutofanyika kwa Mkutano Mkuu na kushindwa kujadili baadhi ya vitu na kuvipitisha kama vile mabadiliko ya Katiba na mengine.