Polisi waelimishwe kukabili msongo

JANA baadhi ya askari wa jeshi la Polisi katika Chuo cha Polisi Kurasini walihudhuria semina ya siku moja iliyoandaliwa na Shirika la Kimataifa la Vijana, IYF, lengo likiwa ni kutoa elimu ya mbinu za kukabiliana na msongo wa mawazo.

Mtoa mada kwenye semina hiyo alikuwa ni mtaalamu wa saikolojia kutoka Korea ya Kusini, Dk Kim Ki Sung ambaye aliwaelekeza askari hao athari za kuwa na msongo wa mawazo, sababu zake pamoja na njia za kuzitatua kero zinazopelekea mtu kuwa na msongo wa mawazo.

Binafsi nimeguswa na mafunzo hayo kwa kuwa ni muhimu hasa kwa Jeshi la Polisi ambalo askari wake ndio wanaohudumia jamii kila siku. Mafunzo haya ni muhimu kwa askari kwa kuwa katika utekelezaji wao wa kazi za kila siku wanakumbana na changamoto kadhaa za kiutendaji ambazo zinaweza kuwafanya kuwa na msongo wa mawazo.

Hapa namaanisha kuwa, askari wanaweza kukumbwa na msongo wa mawazo wakati wowote na hivyo kibarua kilichopo mbele yao ni kuangalia njia gani wanazoweza kuzitumia katika kukabiliana na changamoto hizo.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo amesema, wanatakiwa kutambua kuwa, kazi zao zinahusiana na mambo yanayoweza kuwafanya kuwa msongo wa mawazo na hivyo wasisite kuwasiliana na wakubwa wao au wenzao kutafuta suluhu za kero husika.

Au kama ikishindikana basi ni vema kwa askari kuzivumilia changamoto na kuzichukulia ni sehemu ya kazi huku akizitafutia ufumbuzi taratibu, hii nayo ni mbinu inayoweza kusaidia kuvikabili vyanzo vya msongi wa mawazo.

Kulikubali jambo na kuamua kulitatua wewe mwenyewe au kwa kushirikiana na watu ni njia bora kubwa na sahihi kuliko kuliwekea kinyongo moyoni. Huo ndio mwanzo wa kujikuta askari anaamua kujiua au hata kuwadhuru wengine ili kumaliza hasira.

Ni wazi kuwa katika jeshi la polisi zipo changamoto mbalimbali kama vile ukosefu wa vifaa vya kazi, mishahara, umbali na familia na eneo la kazi, hali ya hewa pamoja na matatizo mengine ya kikazi yanayosababishwa na wakubwa wa kazi au wanajamii.

Ni wazi kuwa iwapo askari wakiwa na msongo wa mawazo kwa muda mrefu wanaweza kuiathiri jamii wanayotakiwa kuihudumia. Hiyo ni kwa sababu msongo huo unawafanya askari kuwa na hasira na kujikuta wakitumia nguvu isiyostahiki katika kuwakabiri waharifu na hata raia wasiokuwa waharifu.

Ni vema kuanzishwa kwa somo la kukabiliana na msongo wa mawazo kwenye mitaala ya vyuo vya Polisi nchini ili liwe endelevu na lenye kuwajenga askari namna ya kukabiliana na msongo wa mawazo tangia wakiwa vyuoni.

Lakini pia wakubwa wa Polisi ngazi za mikoa kuanzisha hata utaratibu wa kuwa na washauri wa masuala ya kisaikolojia kwa askari ili wawe na uhuru wa kwenda na kupewa ushauri wa kikazi.