loader
Picha

Mpango ayashukia rasmi mashirika yasiyotoa gawio

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango (pichani) amesema haridhishwi na mashirika ambayo hayatoi gawio kwa serikali na amemwagiza Msajili wa Hazina, Athuman Mbutuka, kufuta mashirika kama hayo na viongozi wake wawajibishwe.

Alisema hayo Dar es Salaam jana alipofungua Kongamano kuhusu ‘Wajibu wa Mashirika ya Umma katika Utekelezaji wa Ajenda ya Viwanda’. Kongamano hilo liliandaliwa na Taasisi ya Uongozi na washiriki walikuwa wenyeviti wa bodi za wakurugenzi za mashirika na taasisi za umma na watendaji wakuu wa mashirika na taasisi hizo.

“Siridhishwi na mwenendo wa mashirika ambayo hayatoi gawio kwa serikali. Kwa mwaka 2016/17 kati ya mashirika ya biashara 34 yanayomilikiwa na serikali kwa asilimia 100, mashirika 30 hayajatoi gawio. Aidha, kati ya mashirika 36 yanayomilikiwa na serikali kwa ubia na wawekezaji chini ya asilimia 50, mashirika 20 hayajaleta gawio serikalini. Kwa kuwa wakuu wa mashirika husika na Bodi wamo humu ndani, napenda niwaambie kwa lugha kali wajitathmini,” alisema Waziri huyo wa Fedha.

Dk Mpango aliongeza: “Nimemwagiza Msajili wa Hazina achambue na kufuatilia kwa karibu mwenendo wa biashara na uongozi wa mashirika yote ili yale yasiyoenda vizuri, tuondokane nayo na wahusika wawajibishwe. Nimemtaka pia Msajili wa Hazina ahakikishe kila Shirika la Huduma linalotakiwa kuchangia asilimia 15 kwenye Mfuko Mkuu linafanya hivyo bila kukosa”. Waziri Mpango alisema kwa mujibu wa taarifa ya Msajili wa Hazina, serikali ina jumla ya mashirika na taasisi za umma 270, zinazosimamiwa na ofisi hiyo.

Kati ya mashirika hayo, serikali inamiliki mashirika 232 kwa asilimia 100, mashirika mawili kwa zaidi ya asilimia 50 na mashirika manne kwa asilimia 50. Aidha, serikali ni mwanahisa mdogo katika mashirika 32. Alisema idadi hiyo ya mashirika, huenda ikabadilika baada ya kukamilika kwa kazi ya kuunganisha baadhi yake. “Mashirika hayo kimsingi yaliundwa kwa lengo la kutoa huduma kwa haraka na ufanisi, uzalishaji wa bidhaa, kuongeza ajira, kuongeza mapato na udhibiti wa huduma, bidhaa na bei ili kuhakikisha kuwa mwananchi anapata huduma na bidhaa zenye ubora na kwa bei nafuu,” alisema.

Alieleza kuwa serikali inafarijika kutokana na ushiriki wa baadhi ya mashirika ya umma katika uwekezaji wa uchumi wa viwanda. Alisema yapo mashirika yanayowekeza fedha moja kwa moja kama vile mifuko ya hifadhi ya jamii, yapo yanayojenga miundombinu kwa ajili ya kuwezesha ujenzi wa uchumi wa viwanda kama vile Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), Shirika la Reli (TRC), Tanesco na Bandari.

Alisema yapo mashirika mengine mengi, yanayowekeza na kuwezesha kwa njia mbalimbali katika ujenzi wa uchumi wa viwanda. “Yote nayapongeza na kuyataka kuendelea na kazi hiyo nzuri,” alisema. Alisema kiwango kikubwa cha uwekezaji, unaofanywa na serikali kwa mashirika ya umma ni ishara ya imani na matumaini makubwa kwa taasisi hizi.

Aliahidi kuwa serikali itaendelea kuwekeza fedha, kuweka mazingira wezeshi na mifumo saidizi ili kuongeza mchango wa mashirika ya umma katika ujenzi wa uchumi wa viwanda. Dk Mpango alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli, imedhamiria kwa dhati kutekeleza ajenda ya uchumi wa viwanda na mifano michache inathibitisha dhamira hiyo.

Kwanza, serikali imetamka bayana kuwa ujenzi wa uchumi wa viwanda ni ajenda namba moja na imetengeneza mikakati inayotekelezeka ya kuelekea huko. Pili, serikali imeamua kufufua viwanda vilivyobinafsishwa, ambavyo vilikuwa vimekufa au kutofanya kazi. Tatu, serikali imeamua kuchukua viwanda ambavyo wawekezaji wake wameshindwa kuviendeleza na kuwakabidhi wawekezaji wenye uwezo na nia ya kuvifufua na kuviendeleza. Nne, serikali imedhamiria kuwekeza kwa nguvu katika miundombinu wezeshi ya barabara, reli na umeme wa uhakika.

CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) Zanzibar kimesema wakati ...

foto
Mwandishi: Nelson Goima

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi