loader
Picha

Boeing 787-8 Dreamliner kuanza safari wiki tatu zijazo

NDEGE mpya aina ya Boeing 787-8 Dreamliner iliyowasili nchini Jumapili iliyopita na kupokewa na Rais John Magufuli, itaanza safari zake za ndani baada ya wiki tatu kuanzia sasa.

Ndege hiyo ambayo ina uwezo wa kubeba abiria 262, itaanza kazi kwa kufanya safari za ndani ya nchi kwa takribani mwezi mmoja kabla ya kuanza safari za nje ya nchi. Mkurugenzi Mtendaji ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Ndege nchini (ATCL), Ladislaus Matindi, aliliambia HabariLeo jana kuwa sababu ya ndege hiyo kuanza kazi baada ya wiki tatu kuanzia sasa inatokana na matakwa ya kiusalama.

Matindi aliyataja baadhi ya matakwa hayo ya kiusalama ambayo yanapaswa kuzingatiwa kwanza kabla ya ndege hiyo kufanya safari za ndani na nje ya nchi ni pamoja na kutoa mafunzo ya uokoaji kwa wahusika watakaofanya kazi kwenye ndege hiyo. Sababu zingine alizozitaja ni mafunzo kwa ajili ya kukabiliana na majanga, mafunzo kwa wahudumu wa ndege pamoja na ukaguzi wa ndege.

Alisema hayo ni mambo ya msingi ambayo ni lazima yatekelezwa kwanza kwa ajili ya kukidhi matakwa ya kiusalama ya anga. Mkurugenzi huyo Mtendaji na Mtendaji Mkuu wa ATCL, alisema kuwa ndege hiyo itaanza safari za nje ya nchi mwezi Septemba baada ya kukamilisha safari za ndani. Kwa mujibu wa ATCL, baadhi ya nchi ambazo ndege hiyo itaanzia kwa kufanya safari zake ni pamoja na India na China.

ATCL ilisema ndege hiyo itafanya safari zake za ndani katika viwanja vitatu ambavyo ni Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) uliopo jijini Dar es Salaam, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) uliopo mkoani Kilimanjaro pamoja na Uwanja wa Ndege wa Mwanza. Ikumbukwe kwamba, nauli za kuanzia kwa ndege hiyo kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza itakuwa Sh 113,000 pamoja na kodi kwa safari ya kwenda tu, na kwa wale watakao kwenda na kurudi kati ya mikoa hiyo miwili watalipa Sh 206,000 pamoja na kodi.

Kwa abiria watakaosafiri kati ya Kilimanjaro na Mwanza watalipa Sh 93,000 kwa kwenda tu na watakaokwenda na kurudi watalipa Sh 166,000 zote zikiwa ni pamoja na kodi, wakati watakaosafiri kati ya Kilimanjaro na Dar es Salaam watalipa Sh 98,000 kwa kwenda tu, wakati kwenda na kurudi kati ya mikoa hiyo itakuwa Sh 176,000 zote zikiwa pamoja na kodi. Ujio wa ndege hiyo ya Boeing 787-8 Dreamliner, inafanya ndege mpya zilizonunuliwa na serikali zilizowasili nchini kuwa nne, wakati ndege nyingine mbili mpya zimeelezwa kuwasili mwezi Novemba mwaka huu, na nyingine kubwa kama hiyo Boeing kuwasili nchini mwanzoni mwa mwaka 2020.

CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) Zanzibar kimesema wakati ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi