VERONICA Shirima (49), mwanamke mwenye ulemavu wa ngozi aliyepambana kujitafutia kazi ya kuboresha maisha yake bila ya kusubiri utegemezi.

Ni mwanamke kutoka kwenye familia yenye watoto 10, kati ya hao wanne ni wenye ulemavu wa ngozi na sita wakiwa hawana ulemavu wa aina hiyo. Veronica ni mhitimu wa elimu ya Darasa la Saba na mzaliwa kutoka Kijiji cha Mokala, Rombo Mkuu, Mkoa wa Kilimanjaro, alifi ka Mkoa wa Morogoro tangu mwaka 1992 lengo lake lilikuwa ni kutafuta kazi.

Anasema aliamua kutoka nyumbani kwao hadi Morogoro kwa ajili ya kutafuta maisha yake mwenyewe na eneo lake la kwanza kwenda kuomba kazi ni kwa masista wa Kanisa Katoliki Morogoro.

Veronica anasema masista hao walimpokea kwa mikono miwili na walimpatia kazi ya kuwa msimamizi wa mifugo katika Shule ya Wasichana ya Sekondari Bigwa inayomilikiwa na kanisa hilo.

“Nilipokelewa na kufanya kazi kwa juhudi na maarifa yote na hawajaninyanyapaa kwa kweli …nikikaa nikiwa najua nifanye hivi, namie niwe na kwangu na Mungu amenisaidia,” anasema.

Veronica anasema pamoja na kuwa mwanamke mwenye ulemavu, lakini sio kigezo cha kushindwa kufanya kazi na kujitafutia riziki kwa ajili ya kujitegemea kimaisha.

Anasema katika kufanya jambo lolote lile lazima uipende kazi na kujiamini unapopewa kufanya jambo lolote. Veronica anasema baada ya kupata kazi alianza na mshahara wa Sh 5,000 kwa mwezi na aliutumia kwa uangalifu ili ukidhi mahitaji ya msingi kwenye maisha yake.

“Mimi nilipofi ka mjini Morogoro mwaka 1992 na kupata kazi nilikuwa na shauku ya kusema nipate eneo langu la kuishi,” anabainisha alichokuwa amelenga kufanikisha.

Anasema kupitia mshahara huo aliwekeza yaani kwenye kibubu cha kuhifadhi fedha na mwaka 1995 alinunua kiwanja sehemu anakofanyia kazi (Bigwa) kwa Sh 55,000 na kujenga nyumba mwaka 2003.

“Baada ya kujenga nyumba yangu eneo la Bigwa Minarani niliondokana na mambo ya kuishi kwenye nyumba za kota na kuhamia kwenye makazi yangu na ninaendelea na kazi yangu,” anasema.

Kwa mujibu wa Veronica, amekuwa akitumia fursa wanazopewa na serikali na Shirika la Adra Tanzania inayowasaidia watu wenye ulemavu wa ngozi katika kujikwamua kiuchumi.

Anasema kuwa wanawake wenye ulemavu wa ngozi wakipambana wanaweza kusonga mbele na kuondokana na utegemezi kwa watu kwa kutumia kigezo cha ulemavu wao.

“Mimi binafsi nimepambana na nimeweza kusomesha mtoto na ninaendelea kujenga, nina nyumba ya vyumba vitatu,” anasema.

Shirima kwa sasa anazitumia fursa wanazopewa serikali pamoja na Shirika la Adra Tanzania ambalo linawaunganisha ili kuzifi kia fursa za ajira, kujiajiri na amejizatiti na kuwa pamoja na ulemavu wake ameweza kujikwamua kiuchumi.

“Tukiamua tunaweza, tujisogeze mbele na tusiwe tegemezi kwa watu, kwani mimi binafsi kwa kujitegemea nimeweza kusomesha shule mtoto wangu na yupo kidato cha nne na kujenga vyumba ya vyumba vitatu,” anasema.

Veronica anasema wanawake wenye ulemavu wanapaswa kujiamini na kutumia fursa zilizopo za uwezeshaji zinazotolewa na serikali na wadau wengine kuunganisha nguvu kuanzisha miradi ya kujitegemea. Anasema inawapasa kwa umoja wao kuachana na fi kra za kuwezeshwa katika kila jambo.

“Sisi wenye ulemavu hasa wanawake tuache kujiona hatuwezi kufanya shughuli za ujasiriamali, bali inawezekana tukithubutu,” anasema. Veronica anasema Shirika la Adra Tanzania limempatia fedha bila riba Sh 400,000 kuendeleza mtaji katika shughuli za ujasiriamali.

Anasema kupitia fedha hiyo ameanza ufugaji wa kuku 18 na kwamba fedha iliyobakia ameongeza kwenye mtaji wake wa kununulia sabuni za mche kwa ajili ya kukopesha jirani zake.

“Katoni moja ya sabuni inauzwa Sh 75,000 na ninawakopesha wateja wangu kwa Sh 4,000 na ndani ya mwezi mmoja ninapata kiasi cha Sh 100,000 ukitoa manunuzi, faida inayobakia ninaitumia kuhudumia familia yangu,” anasema.

Veronica anasema zamani alikuwa mwoga kwani alikuwa akijinyanyapaa yeye mwenyewe kwa kushindwa kujitokeza mbele ya jamii kwa kuhofi wa watu kumwangalia vibaya.

Anaongeza kuwa lakini hivi sasa anajitambua na yupo katika vikundi, vikoba mtaani na umoja wa wanawake wa waliotoka nje ya Mkoa wa Morogoro cha kusaidiana kwenye shida na raha.

“Haya yote sasa yameniweka nisiwe na woga na ninaweza kusimama mbele ya kikundi na jamii na nimepata uongozi kwenye vikundi na tunashirikiana na wanajamii wengine,” anasema.

Veronica anasema sasa ana elimu ya fedha, kuwa na nidhamu ya fedha na kwamba fedha anayopata inawekwa kwenye mpangilio wa matumizi.

Anasema licha ya miradi mingine, kinachomweka mjini ni ufugaji wa nguruwe ambapo kwa sasa anao zaidi ya watano kwani anapowauza wanamwingizia fedha nyingi.

“Ninawashauri wanawake wenzangu hasa wenye ualbino wasitegemee kuwezeshwa na kuwa tegemezi, fursa zipo nyingi ambazo wakizitumia wanaweza kufi kisha ndoto zao,”anasema.

Anaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka asilimia mbili kwa ajili ya watu wenye ulemavu kwa ajili ya kuwasaidia kujikwamua kiuchumi.

“Ninamshukuru Rais kwa kuweka hii asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu, inatoa nafasi kwa mashirika na taasisi nyingine kuwawezesha watu wenye ulemavu tukiwemo sisi wenye ulemavu wa ngozi,” anasema.

Veronica anawashauri wenye ulemavu wanawake kwa wanaume wajitoe kushiriki kufanya kazi za ujasiriamali kwa kuunda vikundi ama mtu mmoja mmoja ili waondokane na utegemezi.

“Wapo wenye ulemavu wamehitimu elimu kuanzia ya sekondari na vyuo vikuu, sasa wasisubiri kuajiriwa serikalini kwani kuna fursa nyingi na maisha yanaendelea …tena wao wameendelea kuona mbali zaidi tofauti na yeye aliyeishia darasa la saba,” anabainisha.

Veronica anasema wenye elimu wanaweza kutumia fursa nyingi ikiwa ni pamoja na kuandika maandiko ya kuomba mikopo na kuwaelimisha kuondokana na mfumo wa sasa wa kuweka mbele kusaidiwa.

“Kumbe tukiwezeshwa na tukifanya tunaweza kujikwamua kimaisha na mimi ni mmojawapo niliyefanikiwa kwa juhudi zangu,” anasema.

Veronica anawasihi wenzake wasiwe waoga kutumia fursa ya asilimia mbili ya mikopo iliyotolewa na serikali kwani kushindwa kutumia fursa hiyo ni kujikatisha tamaa ya kusonga mbele kimaendeleo.

Kwa upande wa maisha yake binafsi anasema ana mtoto mmoja mwenye umri wa miaka 16 na mwaka huu anahitimu elimu ya kidato cha nne. Veronica anasema aliibeba mimba hiyo na hakuitoa hadi alipojifungua salama mwaka 2005.

“Sikuolewa ila nilibahatika kupata mtoto, nilipopata ujauzito nikamweleza mwenzangu yaani mzazi mwenzagu kuwa nina ujauzito.

“Nikajibiwa na mwezangu kuwa hawezi kwenda kunitambulisha kwa ndugu zake kutokana na hali yangu ya ulemavu wa ngozi,” anasema.

Veronica anasema ilikuwa mimba isiyotarajiwa kwa vile wote wawili walikuwa hawajatambulishana kwa wazazi na ilitokea kama binadamu.

Anamalizia kwa kusema Mungu yu mwema kwa sababu amemuwezesha kujisimamia yeye na mwanawe na kudhihirisha ukiwa na malengo, ukijiamini unaweza kufanikiwa katika jambo lolote katika maisha hata kama una changamoto ya ulemavu.

Habari Zifananazo

Back to top button