loader
Dstv Habarileo  Mobile

Kitaifa

Mpya Zaidi

Wanawake 8,000 hufa kwa ujauzito kila mwaka

Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Kebwe Stephen KebweLICHA ya mafanikio yaliyopatikana Tanzania, bado inakabiliwa na tatizo kubwa la vifo vya akinamama 8,000 kila mwaka kutokana na sababu zinazohusiana na ujauzito, vingi vikiwa vya vijijini.

Hayo yalibainishwa na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Kebwe Stephen Kebwe katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Nkasi , Iddy Kimanta.

Alisema hayo katika sherehe za makabidhiano ya vyumba vitano vya kisasa na vifaa vya upasuaji, zilizofanyika juzi kijijini Mwimbi wilayani Kalambo mkoani Rukwa.

Vyumba hivyo vitano vya kisasa vya upasuaji vimejengwa na Taasisi ya William Mkapa katika vituo vya afya katika halmashauri za Kalambo, Sumbawanga na Nkasi mkoani humo.

“Changamoto kadhaa zinazosababisha hali hii ni pamoja na uhaba wa upatikanaji na ufikaji wa huduma za afya haswa huduma za dharura kabla na wakati wa kujifungua ikiwemo huduma za upasuaji na utoaji wa damu,” anabainisha Kebwe.

Kwa mujibu wa Kebwe ili kufikia lengo la Milenia la kupunguza vifo vya wajawazito kwa asilimia 75 mwaka ujao Serikali imejiwekea mikakati mbalimbali ikiwemo Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) na Mpango Maalumu wa kupunguza vifo vya akinamama na watoto wachanga “Oneplan” .

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Mkapa, Dk Adeline Nyamwihura alibainisha kuwa ujenzi wa vyumba hivyo vitano vya kisasa vya upasuaji vimefuata mwongozo wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Aliongeza kuwa kwa miaka minane Mkoa wa Rukwa umenufaika na miradi mingi inayotekelezwa na taasisi hiyo kupitia mradi wake wa Mkapa Fellows wakiwemo watumishi wa afya 50 ambao wameajiriwa na taasisi hiyo na kuletwa mkoani humo kwa ajili ya kutoa huduma za tiba katika maabara ya Hospitali ya Mkoa , hospitali za Umma za wilaya na Vituo vya Afya vya Serikali.

Pia kwa mujibu wake mwaka jana taasisi hiyo ilikabidhi nyumba za watumishi wa afya 20 kati ya 40 zinazoendelea kujengwa mkoani humo.

zaidi ya miaka 7 iliyopita