Mtwara watakiwa kutunza miundombinu ya barabara

MTWARA; MKUU wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala amewataka wananchi mkoani humo kutunza miundombinu ya barabara  kwa sababu inainua uchumi na kuleta maendeleo kwa kijamii.

Akizungumza mkoani humo, amesema uwepo wa barabara nzuri kuna faida katika masuala ya kiuchumi,  inarahisisha uletaji wa bidhaa mbalimbali sokoni na kuongeza ajira kwa Watanzania kama vile mama lishe na wengine.

‘’Miundombinu hii ikiwa mizuri inakuwa rahisi hata akina mama wajawazito kupata msaada wa haraka katika masuala ya kujifungua, ikiwa mbovu unaweza ukapoteza uhai wa mama na mtoto wake kwa sababu ya kuchelewa kufika hospitalini,’’amesema Sawala.

Meneja wa Wakala ya Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Doto John amesema mkoa huo una jumla ya kilomita 1,313, kati ya hizo kilometa 284 ni barabara kuu ambazo zote ni za kiwango cha lami, kilomita 1,029 za mkoa kati ya hizo kilomita 163 ni za lami, nyingine za udongo ambapo zote zinapitika wakati wa kiangazi na sehemu chache wakati wa masika.

Amesema ukarabati wa kiwanja cha ndege mkoani  humo, ujenzi umeshakamilika na kinatoa huduma saa 24, taa za barabarani 555 zimewekwa katika maeneo mbalimbali ndani ya mkoa.

Ofisa Hifadhi ya Barabara wa Tanroads mkoani humo, Benigna Eriyo amewaomba wananchi hao wasitumie maeneo ya hifadhi ya barabara kufanya shughuli mbalimbali za kijamii, ili kuepuka uharibifu wa miundombinu.

Viongozi hao walikuwa wakizungumzia mafanikio ya miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Habari Zifananazo

Back to top button