loader

Uchumi

Mpya Zaidi

‘Zao la miwa liingizwe katika mfumo wa pembejeo za kilimo

UMOJA wa Wakulima wa Kilimo cha Miwa mkoani Kagera (KASGA) wameiomba serikali kuliingiza zao la miwa katika mfumo wa pembejeo za kilimo ili kupunguza gharama za kununua dawa ambazo ni kubwa na kuwasababishia kushindwa kumudu.

Mmoja wa wakulima hao, Anasi Swaibu alibainisha hayo hivi karibuni mjini Kyaka wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi juu ya changamoto zinazowakabili katika kilimo hicho.

Swaibu alisema sasa wakati umefika Serikali kuliingiza zao hilo katika mfumo wa pembejeo ili kuondoa ukiritimba ambao upo kwa sasa katika maduka ya wauzaji binafsi wa dawa au pembejeo zinazotumika katika kilimo hicho.

Alisema mfano dawa ya kuulia magugu ambayo huuzwa zaidi ya Sh 16,000 kwa lita moja hapa Tanzania wakati nchini Uganda dawa hiyo hiyo huuzwa kwa gharama ya Sh 10,000 jambo ambalo linasababisha wakulima hao kushindwa kulima kilimo chenye tija kilicho bora.

“Gharama hiyo ni kubwa kwa mkulima wa kawaida kama sisi itakuwa vigumu kuendelea, basi Serikali ilione hili la kuweka zao hili katika mfumo wa pembejeo kama yalivyo mazao kama korosho maana tunajikuta asilimi 90 ya faida hiyo inaishia katika ununuzi wa dawa,”alihoji Swaib.

Mkulima mwingine wa miwa, Ahmed Kajubi alishauri kama Serikali haiwezi kuweka utaratibu wa pembejeo za ruzuku katika zao hilo basi viwanda vya sukari nchini viweke utaratibu wa jinsi ya kukopesha pembejeo kwa wakulima hao pale wakipeleka miwa waweze kurejesha au kuwauzia wakulima wadogo pembejeo hizo kwa bei ya kawaida ili waweze kumudu gharama hizo na kufanya kilimo cha miwa kuwa cha uhakika na kupendwa na wakulima wengi.

zaidi ya miaka 8 iliyopita